Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi amekemea mawaidha potofu yanayotolewa na baadhi ya wanazuoni wakiwataka Waislamu nchini kutofundishwa elimu dunia.
Mwinyi alitoa rai hiyo jana, kwenye Kongamano la
Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, lililoandaliwa na Chuo cha Kiislamu cha
Kimisri cha Al-Azhar Shariif, ambalo lilijadili mauaji kinyume cha
Sheria za Kiislamu.
“Elimu ni suala nyeti, tukemee uondoaji wa watoto
wa Kiislamu shuleni na vyuoni kwa uongo kwamba ni elimu ya kikafiri,”
alisema Mwinyi. Aliongeza: “Nastaajabu yanayotendeka Kigoma, hata
yanayofanywa na Boko Haram kwa jina la Uislamu. Uislamu haupiganiwi kwa
kuteka, kunajisi, kuua wala kuwalazimisha wasiokuwa tayari kuufuata.”
Alhaji Mwinyi alijumuika na masheikh pamoja na
wanazuoni wa hapa nchini na Misri kujadili mwenendo wa mauaji
yanayoendelea katika sehemu mbalimbali duniani yakifanywa chini ya
mwamvuli wa Uislamu ambapo walieleza kuwa kila kiumbe kina haki ya
kuishi.
“Kuna taarifa tumezipata kuwa kuna masheikh kutoka
Oman walikwenda Kigoma na kuwaagiza Waislamu wawaondoe watoto wao
shuleni au vyuoni iliwasipate elimu dunia.
Viongozi wa Uislamu tupige kelele kwa kuchukua
hatua thabiti kuiokoa dini yetu kwani Boko Haram walianza kama hiv,i
lakini hakuna aliyewajali wa kidhani kuwa hakuna atakayewazingatia na
kuwasikiliza na sasa wanaleta machafuko Nigeria,” alisema Sheikh Mataka.
Naye Sheikh Suleiman Kilemile kutoka Tandika
wilayani Temeke, alieleza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kusimamia
misingi ya dini hiyo ipasavyo ili kuzuia watu wanaotumia nyumba za ibada
kutoa hisia zao binafsi akisema huko siyo sehemu sahihi.
Naye Sheikh Salah Sayed Hussein Maftaha, raia wa
Misri ambaye pia ni mkuu wa chuo hicho, alisema kuwa wameandaa kongamano
hilo ili kuwapa Waislamu wa Tanzania na Misri fursa ya kujadili na
kulaani upotoshaji wa maadili ya dini unaofanywa sehemu mbalimbali
duniani.
0 comments:
Post a Comment