Thursday 28 August 2014


 “Tunalipa wajumbe wanaohudhuria bungeni, kama hilo linatendeka lazima nilifuatilie. Ninachosema kama kuna waziri amelipwa na hayupo itabidi aturejeshee hiyo fedha. Lakini hili tatizo ni gumu kwa sababu mtu analipwa na tunajua yupo kumbe pengine hajaingia katika vikao
 Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limedai kuwa baadhi ya mawaziri na manaibu wao wamekuwa wakilipwa posho za kuhudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katiba hata wanapokuwa hawapo bungeni.
Kaimu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda alisema jana: “Mawaziri na manaibu ambao ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walioko mjini Dodoma wanapokuwa na safari za kikazi huaga kwa Waziri Mkuu lakini jambo la kushangaza ni kuendelea kulipwa posho wakati hawapo.”
Alisema hali hiyo husababisha Bunge hilo kuendelea kuwalipa posho kupitia akaunti zao za benki lakini wakiwa hawapo Mjini Dodoma. Mwakagenda alisema mawaziri hao wanapotoka kwenda kwenye shughuli mbalimbali za kiserikali nako hulipwa posho.
“Haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma, mawaziri na manaibu wanalipwa posho hata wanapokuwa nje ya Bunge Maalumu la Katiba, wanaposafiri pia wanalipwa posho na Serikali,” alisema Mwakagenda.
Alisema pamoja na kwamba Ofisi Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba imeonyesha kubana mianya kwa wajumbe kusaini bila kufanya kazi, bado kuna ufujaji wa fedha eneo la mawaziri.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema ruhusa za kutoka nje ya Dodoma hutolewa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta na kwamba wasiohudhuria huwa hawalipwi.
“Tunalipa wajumbe wanaohudhuria bungeni, kama hilo linatendeka lazima nilifuatilie. Ninachosema kama kuna waziri amelipwa na hayupo itabidi aturejeshee hiyo fedha. Lakini hili tatizo ni gumu kwa sababu mtu analipwa na tunajua yupo kumbe pengine hajaingia katika vikao,” alisema.
Alisema kanuni za Bunge hilo zinataka mjumbe anapoondoka aombe ruhusa kwa Mwenyekiti wa Bunge na nakala kwa Katibu.
“Wakicopy (wakinakili) kwangu mimi nawaorodhesha nampelekea mhasibu, tukikaribia kulipa namwambia hawa hawapo, kwa hiyo mtu siku ambazo anaomba ruhusa hata kama anaumwa hatumlipi, labda awe amelazwa hospitali ambaye tunamlipa half (nusu),” alisema.
Hata hivyo, alisema tatizo linalowapa shida kiutendaji ni kwa wale wasioaga wanapotoka nje ya Dodoma na kwamba hilo atalifuatilia kwa kuangalia orodha za mahudhurio kwenye vikao.
Mahudhurio hafifu
Kuhusu mahudhurio Hamad alikiri kwamba hilo ni tatizo kutokana na baadhi ya wajumbe kutokuwa makini na kwamba mahudhurio hafifu yanaathiri uendeshaji wa vikao hivyo.

0 comments:

Post a Comment