Pia, ameipongeza iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kuandaa Rasimu bora na kuwaomba
wajumbe wake kuwa na ngozi ngumu ya uvumilivu katika kipindi hiki na
waepuke kurushiana maneno na watu wanaowakejeli.
Jaji Werema aliyasema hayo jana wakati akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea mchakato huo
ulipotoka, ulipofika na unakokwenda huku akitumia Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba na Rasimu ya Katiba kufafanua baadhi ya mambo.
Mwanasheria huyo, akijibu swali aliloulizwa kuwa
Bunge Maalumu la Katiba linaendelea wakati wajumbe kutoka Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiwa hawashiriki, Je, ikishindikana
kupatikana kwa theluthi mbili itakuaje? Alisema: “Katika kamati theluthi
mbili inatosha, lakini kule mwisho (katika kura ya maoni ya kuipitisha
Katiba itakayopendekezwa) kama tutafika darajani, hilo ni suala la siku
za usoni.
“Kama tutafika huko na kukuta hakuna pa kutokea,
tutarudi bungeni (Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na kufanya
marekebisho ya 15 katika Katiba ya sasa ya mwaka 1977 kama uwepo wa Tume
huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi na kupunguzwa kwa mamlaka ya Rais,
vitu ambavyo vimekuwa vikizungumzwa sana na wananchi,” alisema Jaji
Werema.
Kuhusu madaraka ya Rais kulivunja au kulisitisha
Bunge hilo, Jaji Werema alisema “Sheria haimruhusu Rais kulivunja au
kulisitisha na katika maongezi yangu na yeye (Rais Kikwete) nilimweleza
kwamba hana madaraka hayo.”
Aliongeza: “Nimemwambia hana mamlaka ya
kusimamisha, hana mamlaka ya kulivunja na wala asifikirie kwani Sheria
haikumpa mamlaka na akifanya hivyo atakuwa anavunja Katiba.”
Jaji Werema alisema mamlaka ya Bunge hilo
inatokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayolitaka kujadili na
kupitisha Rasimu iliyopendekezwa na Tume kisha kuandaa Katiba na
kuipeleka kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
“Kisheria maana ya kujadili ni kuboresha,
kubadilisha na kuweka jambo vizuri na hii siyo mimi bali tulikubaliana
wote na kanuni zikaandaliwa,” alisema Jaji Werema.
Kuhusu mabadiliko ya kanuni ilizozifanya Bunge
hilo wakati Ukawa wakiwa hawapo alisema: “Tulifanya hivyo kwani Rais
(Kikwete) amesema siku 60 alizoongeza zikiisha hawezi kuongeza tena,
hivyo tumefanya hivyo ili kuwezesha siku hizo zitoshe.”
Aprili 16 mwaka huu, wajumbe wa Ukawa kutoka vyama
vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na baadhi ya wajumbe kutoka kundi la 201
walisusia kushiriki shughuli zote za Bunge hilo hadi pale Rasimu
iliyowasilishwa na Jaji Warioba iheshimiwe kutokana na kubeba maoni na
mapendekezo ya wananchi.
Hata hivyo, Bunge hilo liliendelea na vikao vyake
hadi lilipoahirishwa Aprili mwaka huu kupisha Bunge la Bajeti na Agosti 5
mwaka huu. Lilirejea tena na kuanza vikao vyake huku wajumbe wa Ukawa
wakiwa wameendelea kushikilia msimamo wao.
0 comments:
Post a Comment