Sunday, 24 August 2014

VIONGOZI WAPYA CHADEMA MBINGA WAPEWA SOMO

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Mbinga mkoani   Ruvuma, kimepata viongozi wapya ambao watakiongoza chama hicho wilayani humo baada ya kufanya uchaguzi wake, huku wakitakiwa kufanya kazi bila ubaguzi au upendeleo wa aina yoyote ile.

Aidha viongozi hao waliochaguliwa wameshauriwa kutojenga makundi katika kipindi cha uongozi wao ikiwa ni lengo la kuondoa mipasuko ndani ya chama ambayo inasababisha malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Hayo yalibainishwa na Wajumbe wa mkutano Mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa CHADEMA ngazi ya wilaya ya Mbinga, uliofanyika kwenye ukumbi wa Tulivu uliopo mjini hapo.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mwakilishi wa chama hicho Kanda ya kusini  Menlufu Mapunda, ambapo wajumbe hao kwa nyakati tofauti walisema itakuwa ni jambo la kusikitisha endapo watawaona viongozi wao wakiwatenga katika mambo mbalimbali, huku wakisisitiza ni vyema kuanzia sasa pawepo na mabadiliko chanya ambayo yataleta maendeleo kwa wanachama na chama kwa ujumla.


Naye Mapunda kwa upande wake aliunga mkono hoja za wajumbe wa mkutano huo, akisema ni aibu na dhambi kwa kiongozi aliyewekwa madarakani kutotimiza majukumu yake ya kazi ipasavyo na hatma ya kiongozi wa namna hiyo, ni kuwajibishwa ili iwe fundisho kwa wengine.

“Ndugu zangu nawaombeni sisi wenyewe kwanza ni lazima tujikomboe kifikra, tisijiweke nyuma katika kupigania haki zetu tujitume hasaa”, alisema.

Pamoja na mambo mengine Wajumbe hao wa mkutano mkuu wa uchaguzi kwa ngazi ya wilaya ya Mbinga, waliwachagua viongozi wao ambao watawaongoza katika kipindi cha miaka mitano ambapo Mwenyekiti Kenan Mkuzo alipata kura 78 na kumbwaga chini mpinzani wake Teobard Ndunguru aliyepata kura 24.

Kwa nafasi ya Katibu mkuu wa wilaya hiyo ambayo ilikuwa ikigombewa na mtu mmoja alipita kwa kupata kura 94 za ndiyo na 4 za hapana, huku nafasi ya uenezi ikinyakuliwa na Kelvin Ndunguru kwa kura 98.

Nafasi ya Mweka hazina alichukuliwa na Joyce Malingana kwa kura 63 na kumgaragaza chini mpinzani wake, Anastazia Magubika aliyepata kura 38 ambapo kwa upande wa baraza la wazee Winfrid Ndunguru alipata kura 98 na katibu wake Linus Juma, kura 98.

Baraza la vijana Mwenyekiti aliyeshinda ni Dominicus Njako alipata kura 24 huku mpinzani wake akipata kura 22, katibu wake Benno Fussi kura za ushindi alipata 28 mpinzani wake alimbwaga chini kwa kura 19.

Vilevile kwa upande wa baraza la akina mama mshindi alikuwa Gaudensia Komba alipata kura 19 na katibu wake Magreth Swai aliyepata kura 12, na kwamba katika mkutano huo waliteuliwa wajumbe wawili wa kuwakilisha taifa na wa nne ngazi ya wilaya.

0 comments:

Post a Comment