Rais Kikwete alinukuliwa akisema ndani ya Kamati
Kuu ya CCM iliyomaliza kikao chake juzi mjini hapa kwamba yeye si
kikwazo cha mahudhurio kwenye kamati za Bunge hilo na kwamba hata katika
ziara yake ya Morogoro hawahitaji.
“Mwenyekiti aliweka wazi kabisa kwamba hata katika
ziara yake ya Morogoro watumwe makatibu wakuu wa wizara kama kuna
ulazima huo,” kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo, katika ziara yake mkoani Morogoro
iliyoanza jana, Rais Kikwete aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani ambaye pia ni
Mbunge wa Ulanga Mashariki ziara hiyo ilikoanzia.
Pia alikuwapo Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Stephen Masele ambaye alihudhuria tukio la uzinduzi wa mradi wa umeme
vijijini katika Kijiji cha Mwaya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema: “Kamati Kuu inawahimiza wajumbe
wa Bunge la Katiba, kuhudhuria vikao vya kamati na vile vya Bunge na
kushiriki katika mijadala kwa kutanguliza masilahi mapana ya Taifa na
hatimaye kuipatia nchi Katiba inayotarajiwa na Watanzania wote.
Akifafanua, Nnauye alisema suala la mahudhurio
kwenye vikao lilizungumzwa kwenye CC na kwamba mawaziri na wajumbe
wengine wa Bunge la Katiba, wametakiwa kupunguza utoro ili akidi ya
wajumbe iwe inatimia wakati wa kufanya uamuzi.
Nnauye alisema tatizo la wabunge na mawaziri
watoro katika vikao vya kamati linajulikana hata ndani ya CCM... “Sasa
ni wakati wa kuwaambia kuwa wapunguze kazi zao nje ya Bunge maana suala
la utoro ni kweli linatufikia na wabunge nawasihi sana wasiwe watu wa
kutoka-toka wakati vikao vinaendelea,” alisema.
Akidi vikaoni
Suala la akidi limekuwa likikwaza kamati za Bunge
Maalumu kiasi cha kusababisha baadhi kuchelewa kuanza kwa vikao na
wakati mwingine kuahirishwa.
Kadhalika, baadhi ya ibara kwenye Rasimu ya Katiba
zimekuwa zikikosa akidi ya theluthi mbili ya kura kutokana na utoro wa
baadhi ya wajumbe, wakiwamo mawaziri ambao mara kadhaa wamelalamikiwa na
wenyeviti wa kamati kwa kutohudhuria.
Agosti 18, mwaka huu Kamati namba 11 ililazimika
kuweka kando kazi zake na ikafanya kile ilichokiita semina ya uelewa kwa
wajumbe, baada ya akidi kutofikiwa.
0 comments:
Post a Comment