Yapo mambo ambayo ubongo wa binadamu unatakiwa kuyafanya kwa ufanisi ili mtu aonekane kuwa ana akili.
Mambo hayo ni kama vile kuwa na uwezo wa kujifunza
na kuelewa kwa haraka, kutunza kumbukumbu na kuwa na uwezo wa kutumia
tena taarifa zilizotunzwa katika ubongo ili kuzichanganua kulingana na
hali halisi ya mazingira yanayomkabili.
Tunaweza kuutazama ubongo kama ilivyo kompyuta
ilivyo na mfumo tata wa kuchakata taarifa ambayo utendaji wake hutegemea
uwezo wa mtumiaji.
Hivyo ndivyo pia ilivyo akili ya binadamu. Akili
hutegemea maumbile ya vitu vilivyomo ndani ya ubongo na mazingira ya
nje,” anasema Dk Mohana Ali katika makala yake ya ‘The
Biological-Environmental Hypothesis of Human Intelligence’
iliyochapishwa Julai, 2014 katika mtandao wa www.dana.org
Katika ubongo kuna nyaya zinazosafirisha taarifa
kutoka seli moja kwenda seli nyingine ya ubongo. Nyaya hizi zimefunikwa
na utando wa mafuta mafuta unaojulikana kama myelin.
Myelin kama ilivyo kwa vifuniko vya plastiki
vinavyofunika waya wa umeme, huzuia mkondo wa taarifa katika seli za
ubongo zisivuje na kwa maana hiyo huziwezesha kusafiri kwa haraka katika
sehemu mbalimbali za ubongo.
Ubongo wenye myelin yenye ubora wa hali ya juu husaidia mtu kuwa na uwezo mkubwa wa kiakili.
Yapo mambo ambayo yanasaidia ubongo kuwa na afya
nzuri na yanasaidia myelin kuwa katika hali nzuri. Ubongo unahitaji
lishe bora na kuchangamshwa ili uweze kufanya kazi vizuri na kuwa na
uwezo wa kiakili. Kwa maana hiyo akili zinalelewa na kukuzwa.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa lishe yenye kiasi cha kutosha cha wanga na sukari ni muhimu kwa ajili ya kuupatia ubongo nguvu.
Ulaji wa samaki pia husaidia ubongo kupata mafuta mafuta ambayo ni muhimu kwa ajili ya kukuza uwezo wa kiakili.
Kucheza, kufanya mazoezi na kuvuta hewa safi ya
kutosha pia ni muhimu kwa ajili ya kuchangamsha akili na kuongeza uwezo
wa ubongo kufanya kazi zake kwa ufanisi.
“Akili yako inahitaji mazoezi pia. Kama utaacha
kujizoeza na kutumia uwezo wa akili na ujuzi wa kutatua matatizo, uwezo
wa kufikiri na utambuzi wa mambo, utategemea vipi akili yako kuwa
nyingi?” anauliza mtaalamu wa tiba ya tabia katika mji wa Florida nchini
Marekani, Andrea Kuszewski.
0 comments:
Post a Comment