Sunday, 24 August 2014


Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akipiga kura wakati wa Mkutano Mkuu wa chama hicho huku akiwa jirani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Picha ya Maktaba
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameingia rasmi katika mbio za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatua ambayo imebadili mwelekeo wa kinyang'anyiro cha nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015.
mtandao huu umethibitisha kwamba Pinda tayari ameamua kujitosa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM ambayo tayari inawaniwa na makada wa chama hicho wasiopungua 15 na baadhi yao wameishatangaza nia zao kwa nyakati tofauti.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema uamuzi wa Pinda kuwania urais mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwakani, umesababisha kiwewe miongoni mwa wagombea na kunakifanya kinyang'anyiro hicho kuchukua sura mpya.
Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliliambia gazeti hili siku chache zilizopita mjini Dodoma kuwa: "Na sisi tumesikia kwamba PM (Waziri Mkuu) amejitosa na kama ni kweli atawasumbua wagombea wengi kutokana na rekodi yake hasa katika uadilifu."
"Yeye (Pinda) ana faida tatu kubwa; kwanza hana kundi katika chama, anaelewana na watu wote, pili nafasi yake ya uwaziri mkuu inampa nafasi ya kufahamika kwa watu wengi na tatu rekodi yake ya uadilifu, hana kashfa za ovyoovyo, labda kama ataharibu dakika hizi za mwisho," alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Wengine ambao wamekuwa wakitajwa kuwania uraia kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.(P.T)
Wegine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta. Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Katiba, Asha-Rose Migiro.
Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Balozi Ali Karume.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema wingi wa wanaojitokeza kutaka kuwania urais ni njia ya kuunda mtandao utakaomwezesha mtu fulani au mmoja kunyakua tiketi hiyo.
"Watu wanapiga kampeni katika harambee kwa njia ya kutengeneza mitandao, kwani ukifika wakati wa chama kumpitisha mgombea, asiposhinda ataibuka na kuwaeleza kuwa mnaoniunga mkono mimi muungeni fulani," alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema kujitokeza kwa idadi kubwa ya wanaowania nafasi ya urais, kutatoa fursa ya wananchi kutambua udhaifu wa kila mmoja jambo litakalowezesha kupatikana kwa mtu sahihi wa kupeperusha bendera ya chama hicho.

0 comments:

Post a Comment