Fatuma Misango
Fatuma Misango mwenye mtandio mweusi kichwani akizungumza na mmoja wa wanawake waliotendwa.
Safari ngumu ya mwanaharakati mwanamke mzaliwa wa Namtumbo,  Mratibu wa  Kituo cha wasaidizi wa sheria Songea, Bi. Fatuma Misango katika harakati za kupigania haki za wanawake, watoto na  kupinga ukatili wa kijinsia.
“Mimi naitwa  Fatuma  Misango, ni Mratibu  wa  kituo cha  wasaidizi  wa sheria kiitwacho Songea Paralegal  Center  (SOPCE),” Bi  Fatuma alianza kujieleza  kwa mwandishi wa makala haya ofisini kwakemjini Songea.
Bi. Fatuma Misango anasema yeye ni  mzaliwa  wa wilaya  ya  Namtumbo mkoa  wa  Ruvuma, mwenye  umri  wa miaka takribani  hamsini sasa.
Anasema alikwama kuipata elimu yake kwamfululizo enzi hizo kutokana na majukumu ya kifamilia, lakini aliamua  kujiendeleza mwenyewe akiwa mtu mzima. Sasa ana elimu ya sekondari  kidato cha nne inayomsaidia sana katikakutekeleza majukumu yake katika kuwasaidia wanawake, watoto na wanaume wenyeuhitaji hasa wanaoteseka na ukatili wa kijinsia majumbani na sehemu za kazi
Kuhusu maisha, Mama  Misango amejaliwa  kuolewa na  kupata watoto wanne na  mume wake  ambaye  anaye mpaka sasa.Katika   safari ya maisha yake alifanikiwa  kufanya  kazi kama karani katika Kampuni  ya Tumbaku  mjini Songea.
Hata hivyo, mama  huyu , alikuwa anashauku na kiu ya  kujiendeleza, hivyo  aliamua kuanza masomo ya uuguzi ambapo alifanikiwa na  kuhitimu masomo hayo  kwa  mwaka mmoja.
Bi. Misangu, hakuridhika na  fani  ya uuguzi tu, hivyo  akajiingiza katika masuala ya siasa na kuwa Diwani  viti maalumu kupitia CCM.
“Hapo ndio  nikaanza  kuangalia ni masuala gani ambayo  nitaweza  kusaidia jamii na hususani wanawake na watoto,” anasema Bi.Misango na kufafanua kuwa baada   ya  hapo, “nikapata mafunzo  ya  sheria kama  kiongozi  yaliyoendeshwa  na  Shirika lisilo la kiserikali liitwalo Mtandao wa Jinsia Tanzania  ( TNGP)  mwaka 2002,”.
Mafunzo ya TGNP  yalimpatia msukumo mkubwa  na  hamasa kuweza  kuanza kuwasaidia wanawake kwa masuala ya  sheria.
Bi. Misango anasema,wanawake  wengi wakipata matatizo  wanakuwa  hawana pakwenda  kueleza  matatizo yao.
Shirika   la TGNP  linalosimamia mambo ya Jinsia na na kutetea haki za binadamu hasmasuala ya sheria  walimwaalika tena  kwenye semina   jijjini Dar  es salaam , baada ya kuona  ana  mwelekeo mkubwa katika  uchangiaji wa mada mbalimbali hasa za utetezi wa wanawake.
Alipokuwa kwenye semina  hiyo, ndipo alipokutana na maafisa wa Shirika ambalo lilimtakawashirikiane  katika kazi  ya kisheria au msaada wa sheria kwa  wanawake   katika  mkoawa Ruvuma , shirika hilo linaitwa Women Legal Aid  Centre  (WLAC) 
Bi.Misango akaanza ukurasa mwingine wa  kushirikisha watu  wengine   na kufungua Kituo   cha  wasaidizi wa Sheria Songea, Songea Paralegal Centre   (SOPCE)  kwa msaada mkubwa wa WLAC  na yeye akiwa ni Mkurugenzi wake.
Walengwa  wa  Kituo hicho hasa, ni wale  wa kipato cha chini  ambao hawawezi   kusimamiwa mashauri yao na  Wakili kwa malipo ya fedha.Hivyo,  walengwa wa jinsi zote  awe mwanamke aumwanaume  hupewa msaada na kituo hicho.       
“Msaada wetu  unakuwa  ni bure, japokuwa  lengo letu hasa ilikuwa ni wanawake na watoto zaidi,” anasisitiza Bi. Misangu .
Shirika la SOPCE tangu lilipoanzishwa  mwanzoni mwa miaka ya  2000,limeweza  kuwasaidia  watu takribani  elfu tano (5,000).
Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Lihangweni, Songea Bi. Maria Komba, anatoa ushuhuda alivyosaidiwa na SOPCE. “Mimi  ni mmoja wapo  niliyepata  msaada wa kisheria  kutoka  SOPCE baada   ya   kunyang’anywa  ardhi  na kijijii  cha Lihangweni , na hatimaye  nikarudishiwa ardhi yangu licha ya umasikiniwangu unaonikabili,” anasema Bi. Maria Komba  .
Ushuhuda mwingine ni ule wa migogoro inayosumbua sana familia hasa ndoa. Bw. Dranus Tadei Njajula anasema bila msaada  wa Mkurugenzi wa SOPCE, ndoa yake  ingekuwa  tayari  imevunjika,  lakini  walimpatia msaada mkubwa  sana na sasa  ndoa  yake imenusurika kuvunjika. “Hawawamenisaidia sana kisheria,  ndoa yangu  sasa ni shwari” anajigamba Bw. Njalula.
 Kwa kuona  kazi  nzuri SOPCE  Na  mkurugenzi wake  Fatuma Misangu,  serikali ya  mkoa  imekisaidia kituo  hicho kwa kuwapatia  ofisi bila malipo  yoyote.  Zaidi ya hapo wateja  wengi wanatoka ofisi ya   mkoa  na ofisi  ya wilaya  ya Songea   vijijini.
Mama Misango  alieleza kesi  wanazo kutananazo  zaidi  ni kesi za ndoa  “wanandoa  wengi sana  wana  migogoro katika  ndoa  zaona mara  nyingi  sababu ni haliduni  ya  kiuchumi”.
Kesi  nyingine  wanayo  kutana  nayo sana ni  ukatili  wa  watoto  “wanawake  wanafanya  ukatili  kwa  watoto  wao  kama  kuwachoma  moto  mikono ukiuliza  sababu eti kaiba  shilingi mia  mbili  tu”. Mama
Misangu  alibainisha  kuwa   sababu kubwa  ni  kuchoka  maisha  ya  shida  na mara nyingine  kutelekezwa  na  waume zao,  hivyo  kupelekea  msongo  wa  mawazo.
Mara  nyingi hamna  kazi au  shughuli  isiyo kuwa na faida  na  changamoto.  “Nilipata  tuzo ya amani  2005  iliyo  julikana  kama  ONE  THOUSAND  PEACE  WOMEN  ACROSS  THE GLOBAL.  Kati  ya watu  elfu  moja  duniani  waliopendekezwa  basi  na mimi  nilikuwemo,” anasema Bi Misango na kwamba faida nyingine ni  kuwa maarufu.
Changamoto  wanazo  kabiliana nazo,  ni pamoja  na  wateja   wao  wengi kuwa  wa kipato cha chini,  nao mara  nyingi  wanaamini  pia kupata  msaada  wa  fedha kutoka  SOPCE. Changamoto  hiyo  inasumbua kwasababu  shirika  la SOPCEhalina fedha za kuwahudumia watu kutatua matatizo yao.
Kuhusu malengo  ya  baadae,  SOPCE  inatarajia  kuona  jamii  yote ya  mkoa  wa  Ruvuma  inaheshimu haki  za  binadamu  hususan  kwa  wanawake  na  watoto.     Pia  wanataka  wanawake wanasimama  wenyewe  katika  kutetea  haki  zao.
Mama  Misango  alitoa ushauri  kwa  wanawake  wajiunge  katika  vikundi mbalimbali   vyaujasiriamali  ili  waweze  kujikimu kimaisha.  Kuishi  bila  kujishughulisha  kuna sababisha kukata tamaa  na  wakati  mwingine  kuamua  kufanya  ukatili  kwa  watoto  wao wenyewe .Biashara  ndogondogo  zinaweza  pia kuwakwamua   kimaisha .