Wednesday, 27 August 2014



Ofisi ya Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, imefafanua juu ya kuchelewa kwa posho wa wajumbe wa bunge hilo, ikisema zilichelewa kutokana na sababu za kiutaratibu wa fedha na kwamba kwa sasa hakuna mjumbe anayedai posho.
 
Ufafanuzi huo ulitolewa jana na Mkurugenzi wa Habari na Itifaki wa Bunge, Jossey Mwakasyuka.
 
Alisema taarifa hizo ni za upotoshaji na zina lengo la kuwadhalilisha wajumbe kufanya waonekane wanaishi kwa kutegemea posho hizo.
 
“Ni vema ikaeleweka kwamba wajumbe wa Bunge Maalum wote ni watu wenye nafasi zao katika jamii na ni wenye kazi au shughuli zao mahususi zinazowaingizia kipato na kwamba Ujumbe wa Bunge Maalum ni nafasi ya muda tu ya kutimiza jukumu la kuliandalia taifa Katiba Mpya,” alisema Mwakasyuka.
 
Alifafanua kwamba wajumbe wote  wanaohudhuria  vikao vinavyoendelea wamekwishalipwa posho zao zote kama wanavyostahili.
 
“Ni vyema ikaeleweka kwamba malipo ya posho yanafuata taratibu za fedha za umma na yanapita kwenye mchakato maalumu unaojumuisha kupata orodha za mahudhurio ya wajumbe kwenye kikao, upatikanaji wa fedha kutoka Hazina, na upatikanaji wa fedha kutoka Benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku kadhaa hadi kukamilika,” alifafanua Mwakasyuka.
 
Aliwahadharisha waandishi wa habari kwa kusema; “Kumbukeni kuwa wajibu wenu ni kuhabarisha umma na sio kupotosha umma na hata kuleta usumbufu kwa jamii kutokana na uandishi usio makini.”

0 comments:

Post a Comment