Friday, 5 September 2014


WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Magufuli amewataka wahandisi kujenga ushirikiano ili kuhakikisha kuwa wanafanikiwa katika kupata miradi mbalimbali ya ujenzi ambayo inatolewa na Serikali.
Magufuli ametoa rai wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa Bodi ya Wasajili ya Wahandisi (ERB)  uliofanyika jana katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Alisema ni vema wahandisi wote ambao wamepata usajili baada ya kula kiapo kuwa na umoja ili kuhakikisha kuwa miradi inayotolewa na serikali wanaipata kwa kutokufanya hivyo kutachangia kuikosa.
Katika mkutano huo zaidi ya wahandisi 250, wataalamu na washauri waliapa katika mkutano huo ikiwa ni baada ya kupata usajili kupitia ERB.
Waziri Magufuli alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kuhakikisha kuwa fedha zote ambazo zinapatikana katika mfuko wa barabara zinatumika kwa kuwapatia wahandisi wa ndani ambao watapata miradi.
“Napenda kutumia nafasi hii ya kufunga mkutano huu kwa kuwaomba muungane katika baadhi ya miradi ambayo inatangazwa na serikali kama wenzenu wanaofanya kule katika daraja la Mmbutu Igunga Tabora ambao umeonyesha mafanikio makubwa”,alisema.
Dk. Magufuli alisema Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano wa aina yoyote ili kuhakikisha kuwa wahandisi wa Kitanzania wanafaidika na kodi zao kwa kupata zabuni ambazo watakuwa na sifa nazo.
Kwa upande wake Msajili wa (ERB) Mhandisi Stephen Mlote alisema kwa sasa jumla ya wahandisi wataalamu na washauri 13826 wamesajiliwa na makapuni 261pamoja na kula kiapo cha kazi hiyo.
Mlote alisema pia hadi kufikia sasa jumla ya wahadisi 330 wamefutiwa usajili pamoja na kampuni 32 ambazo zimeonekana kukiuka kanuni za ERB na kiapo walichoapa.
Alisema pamoja na idadi hiyo bado nchi ina kabiliwa na uchache wa wahandisi wataalamu na washauri ambapo kwa sasa ni sawa na 0.2 asilimia ya watanzania wote hali ambayo ni kinyume na nchi zilizoendelea.
Alitolea mfano nchi ya Australia ambayo ni asilimia0.4, Malaysia 0.13, Uingereza 0.8 na Japani ni asilimia 1 hivyo juhudi zinahitajika zaidi ili kuakukisha kuwa vijana wengi wanahamasishwa kusoma masomo ya sayansi.
Msajili huyo alisema ERB pia inajitahidi kuwatafutia vijana waliosoma fani ya uhandisi ajira ambapo hivi karibuni vijana 448 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali hapa nchini.
Aidha Mlote alisema changamoto nyingine ni wahandisi kukimbia fani hiyo na kujihusisha na fani nyingine kwasababu ya kufuata maslahi mazuri ambayo yanapatikana katika sekta zingine.
Changamoto nyingine ni kuwepo kwa utamaduni wa watanzania walio wengi kutotaka kutumia wahandisi katika ujenzi jambo ambalo linawakatisha tama wahandisi kwani wajenzi hutumia mafundi wamitaani.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ( ERB) Profesa Ninatubu Lema aliwataka wahandisi kuzingatia misingi ya kazi yao ili wawe watu wenye kuchangia uchumi wan chi kwa kazi ambazo wanazifanya.
Lema aliwataka kuzingatia mambo yafuatayo ambayo ni kuchagua, kupanga, kipaumbele, kutekeleza, kufuatilia na kutathimini wakati wanatekeleza miradi mbalimbali ya hapa nchini ili kufikia lengo la Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

0 comments:

Post a Comment