Sunday, 31 August 2014


BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA), limetangaza mfumo mpya wa upangaji wa madaraja ya ufaulu kwa kutumia wastani wa pointi (GPA) ambao utaanza kutumika katika mtihani wa kidato cha nne 2014 na cha sita 2015.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alisema kuwa mfumo huo umekuwa ukitumika katika kupanga madaraja ya ufaulu katika baadhi ya mitihani inayosimamiwa na baraza hilo.

Alisema manufaa yake ni kuwa na mfumo wa kutunuku matokeo wa ina moja katika ngazi zote za mafunzo kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu; matokeo yaliyo katika mfumo huo kwenye cheti yatarahisisha kazi ya udahili wa watahiniwa unaofanywa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na NACTE katika ngazi za juu za mafunzo.

Pia aliongeza kuwa mfumo wa GPA ni rahisi kuelewa kwa wadau wa kada mbalimbali kwa sababu hutoa tafsiri yenye kuonesha mtahiniwa aliye na GPA kubwa ndiye aliye na maokeo mazuri.

Kwa mujibu wa Dk. Msonde, madaraja katika mfumo wa GPA hupangwa katika utaratibu wa Distinction, Merit, Credit na Pass ambapo daraja la juu ufaulu ni Distinction na la chini ni Pass.

Kulingana na utaraibu huo, daraja la Distinction litakuwa na alama kati ya 3.6-5.0, Merit 2.6.3.5,Credit 1.6-2.5, Pass 0.3-1.5 na Fail 0.0-0.2 kwa matokeo ya kidato cha nne wakati wa kidato cha sita Distinction ni kati ya 3.7-5.0, Merit 3.0-3.6, Credit 1.7-2.9, Pass 0.7-1.6 na Fail 0.0-0.6.

“Ukokotoaji wa wastani wa pointi (GPA) ya mtahiniwa hufanywa kwa kuzingatia masomo ambayo mtahiniwa amefaulu. GPA anayopata mtahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne hutokana na wastani wa pointi alizopata katika masomo saba aliyofaulu vizuri wakati kwa kidato cha sita ni masomo matatu,”alisema.

0 comments:

Post a Comment