Tuesday, 19 August 2014


Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimjulia hali Marehemu mwenyekiti mstaafu wa tume ya Uchaguzi JAJI Lewis Makame enzi za  uhai wake alipokuwa amelazwa katika hospitali ya AMI iliyoko Mikocheni jijini Dar es Salaam leo.
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Lewis Makame, amefariki dunia katika Hospitali ya Ami Trauma Centre iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.
Jaji Makame alifariki jana mchana katika hospitali hiyo, alikokuwa amelazwa ambapo pia Rais Jakaya Kikwete, alimtembelea kumjulia hali. Taratibu za mazishi zilikuwa zikiendelea jana nyumbani kwake Masaki.
Historia fupi iliyopatikana, inaonesha kuwa Jaji Makame alikuwa na Shahada ya Kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha London nchini Uingereza, ambapo baada ya kufanya mazoezi na kufanya kazi nchini humo, alirejea nchini Tanzania miaka ya 1960 na kutumikia Taifa mpaka alipofikia cheo cha Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Mbali na cheo hicho, Jaji Makame pia alitumikia Taifa katika nafasi ya Mwenyekiti wa NEC na Mwenyekiti wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa Jumuiya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-ECF).
Wakati akiwa Mwenyekiti wa NEC kwa takribani miaka 19, Jaji Makame aliweka historia ya kusimamia uchaguzi kadhaa wa vyama vingi nchini.
Alistaafu wadhifa huo baada ya mkataba wake kuisha Julai mwaka 2011. Nafasi yake ilichukuliwa na Jaji mstaafu Damian Lubuva.

0 comments:

Post a Comment