Friday 22 August 2014

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imezifuta rasmi ajira 200 za nafasi ya Konstebo na Koplo wa Uhamiaji baada ya kupokea ripoti ya Kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma za upendeleo katika ajira hizo ikidaiwa baadhi ya walioitwa katika ajira ni watoto wa jamaa, ndugu na Maofisa wa Idara ya Uhamiaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, alisema baada ya waombaji wa nafasi hizo kufanyiwa usaili na kuitwa kazini, ziliibuka tuhuma mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Tuhuma hizo zilihusu upendeleo wa ajira hizo kwa ndugu na jamaa za watumishi wa idara hiyo hivyo Wizara ililazimika kuzisitisha na kuunda kamati ndogo ya watu watano ili iweze kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo.

Aliongeza kuwa, kamati hiyo ilipewa siku 10 kuanzia Agosti mosi mwaka huu iwe imekamilisha kazi hiyo ambayo waliifanya kwa muda waliopewa na kutoa matokeo.

"Katika uchunguzi wao, kamati imebaini kuwa, baadhi ya wasailiwa waliolalamikiwa wamethibitika kuwa ni watoto wa ndugu au jamaa wa watumishi wa idara hii.

"Baadhi ya waombaji wa nafasi hizi, walikuwa na umri mkubwa zaidi ya ule uliotajwa kwenye matangazo ya kazi (Konstebo miaka 25 na Koplo miaka 30), lakini walisailiwa na kuitwa kazini," alisema Abdulwakil.

Alisema baadhi ya wasailiwa waliopata alama za juu katika ufaulu hawakuitwa kazini na hakuna sababu maalumu ambazo zimetolewa ambapo matangazo ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari, yalikuwa ya jumla na hayakuainisha viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza kidato cha nne na sita.

Abdulwakil aliongeza kuwa, kutokana na matokeo ya uchunguzi huo, ajira hizo zimefutwa na zitatangazwa upya ambapo mchakato wa ajira utasimamiwa na Wizara hiyo ambapo hatua hiyo pia inahusu ajira 28 zilizokuwa zimetangazwa na kujazwa kwa upande wa Ofisa Uhamiaji Zanzibar.

Aliongeza kuwa, awali ajira hizo zilitangazwa na Kamishna wa Uhamiaji katika gazeti la Serikali Februari 17 mwaka huu na kutoa tangazo hilo kwenye tovuti ya Wizara na Idara ya Uhamiaji.

"Baada ya kutangazwa ajira hizi, maombi 15,707 yalipokelewa na waombaji 1,005 waliitwa katika usaili kati yao, 200 walishinda na kuitwa kazini lakini baada ya kutoa tangazo la kuitwa kazini, malalamiko yalitolewa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa walioitwa katika ajira hizi ni watoto wa jamaa na ndugu

0 comments:

Post a Comment