Mtaalamu kutoka Idara ya Nishati
iliyopo chini ya Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Nyaso Makwaya
akisisitiza jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada kuhusiana na
mikakati ya Wizara katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
……………………………………………………………………………………….
Wizara ya nishati na madini
inatarajia kuanzisha mpango wa taifa wa matumizi bora ya nishati
unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mara baada ya maandalizi yake
kukamilika.
Akizungumza katika kongamano la mabadiliko ya tabianchi
lililokutanisha wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini,
Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
linaloendelea mjini Morogoro, Mhandisi Nyaso Makwaya kutoka Idara ya
Nishati, Wizara ya Nishati na Madini alisema kuwa mpango huo uko katika
hatua za mwisho za ukamilishwaji wake.
Mhandisi Makwaya alisema kuwa maandalizi ya mpango huo yalianza
mwaka 2013 na kuongeza kuwa lengo la mpango huu ni kuweka malengo ya
kitaifa kwa kila sekta kwa ajili ya matumizi bora ya nishati,
kuzichanganua changamoto zilizopo za matumizi bora ya nishati na
kuzitafutia utatuzi na kuandaa miradi ya matumizi bora ya nishati.
“ Nishati ya umeme ni muhimu sehemu yoyote, inahitaji usimamizi
bora hivyo mpango huu unalenga kuboresha matumizi ya nishati katika
sekta zote nchini, iwe viwanda, kilimo, ujenzi,mawasiliano n.k, mpango
huu unatoa dira sahihi kwa kila sekta” Alisema Mhandisi Makwaya
Mhandisi Makwaya aliongeza kuwa mpango huu utapelekea
uanzishwaji wa sheria na kanuni katika usimamizi wa matumizi bora ya
nishati.
Aliongeza kuwa wadau na watekelezaji wakuu wa mpango huo ni
Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka
ya Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Shirika
la Taifa la Viwango (TBS) ambao watajengewa uwezo na mradi huu.
Akizungumzia changamoto zilizopo katika usimamizi wa matumizi
bora ya nishati Mhandisi Makwaya alieleza kuwa ni kutokuwepo kwa kanuni
zinazosimamia matumizi bora ya nishati katika ujenzi na matokeo yake ni
wajenzi kujenga majengo yasiyokuwa na uwiano kati ya ukubwa wake na
kiasi cha nishati ya umeme kinachohitajika.
Mhandisi Makwaya alisisitiza kuwa changamoto hiyo ilipelekea
Wizara kubuni mkakati huo ambao utaisaidia nchi kuokoa kiasi cha nishati
kinachopotea na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa mpango huo elimu
kwa umma itatolewa ili wananchi wawe na uelewa wa kusimamia vyema
matumizi bora ya nishati .
“Wananchi wengi hususani wafanyakazi maofisini na viwandani
hawana uelewa juu ya matumizi sahihi ya nishati ya umeme, mpango huu
utakuwa ni mkombozi na hii itachangia uchumi wa nchi kukua kwa haraka
kwa kuokoa gharama zisizo za lazima. “ Alisisitiza Mhandisi Makwaya
Na Greyson Mwase, Morogoro
0 comments:
Post a Comment