Friday, 22 August 2014

Baraza Kuu la Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Arusha limemtimua katibu wake wa mkoa, Gerald Mwadalu kwa tuhuma za ubadhirifu.

Pia, limemtaka katibu wa CCM wa mkoa, Mary Chatanda, kuacha kuivuruga jumuiya hiyo.

Akisoma uamuzi wa kikao cha baraza hilo mkoani hapa, katibu wa UVCCM wa Wilaya ya Karatu, Alli Rajabu alisema kuanzia jana nafasi ya Mwadalu itakaimiwa na Daniel Kiyongo hadi hapo makao makuu ya UVCCM watakapomteua katibu mwingine.

Rajabu alisema Baraza pia limetoa onyo kwa Chatanda kutoingilia jumuiya hiyo, na kumtaka abaki kama mshauri kupitia vikao vya jumuiya ambavyo hushiriki akiwa mjumbe kutokana na nafasi yake.

“Chatanda, licha ya kuwa mjumbe, huwa hahudhurii vikao vya jumuiya, inapoibuka migongano ndipo huibuka na kupingana na hoja za viongozi kama ilivyotokea katika mgogoro wake na aliyekuwa mwenyekiti wa jumuiya hii, James Millya,” alisema Rajabu.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jana, mwenyekiti wa UVCCM mkoani hapa, Robinson Meitinyiku alisoma tuhuma mbalimbali zinazomkabili katibu huyo, akimtuhumu Chatanda kuwa alikuwa akimlinda.

“Nitoe rai kwa walezi wa chama hasa katibu wa CCM mkoani hapa kuwa awe na roho ya ujasiri wa kuilea jumuiya bila kubagua. Haiwezekani leo mtu awe mbadhirifu halafu tuendelee kumtetea.

“Chama ni chetu sote, hakuna sisimizi wa kuonewa wala tembo wa kuogopwa, kikubwa ni kuheshimiana na kuheshimu utaratibu wote wa chama pamoja na kanuni,” alisema Meitinyiku.

Hata hivyo, Mwadalu alikanusha kuhusika na ubadhirifu na kueleza kuwa chanzo cha yeye kutimuliwa kinatokana na makundi.

Alisema kumekuwa na misuguano ya muda mrefu baina yake na viongozi wenzake ambao wanaonyesha kuegemea katika makundi ambayo hata hivyo hakuyataja moja kwa moja.

Juhudi za kumpata Chatanda, ambaye anahudhuria vikao vya Bunge la Katiba, zilishidikana jana. Hata hivyo, katibu mwenezi wa CCM mkoa, Isack Joseph alikiri kupata taarifa za mgogoro wa UVCCM.

Alisema uongozi wa mkoa utakutana na viongozi wa jumuiya hiyo Agosti 23.

0 comments:

Post a Comment