JESHI la
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetumia mabomu ya machozi
kuwatawanya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), waliokuwa wakizuia
gari la polisi lililokuwa limebeba mtuhumiwa wa kutishia kuua albino kwa
maneno.
Tukio
hilo lilitokea jijini Dar es Salaam jana, ambako albino hao walivamia
gari hilo na kuwataka askari polisi wamshushe ndani ya gari mtuhumiwa
huyo aliyetambulika kwa jina la Ombeni Michael, ili wafahamu alikokuwa
akipelekwa.
Vurugu
hizo zilianza katika Mahakama ya Mwanzo Buguruni, ambako albino
hao walivamia wakati kesi dhidi ya mtuhumiwa huyo ikiendelea katika
mahakama hiyo.(I.N)
Baada ya
kusikilizwa kwa kesi hiyo na dhamana kuwa wazi kwa mujibu wa sheria,
watu hao wenye ulemavu waliamsha hasira ya kupinga kupewa dhamana kwa
mtuhumiwa huyo.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 3, mwaka huu.
Mwekahazina
wa Chama cha Albino Tanzania, Abdillah Omary, alilazimika kuandika
barua mahakamani hapo kupinga hatua ya kupewa dhamana kwa mtuhumiwa
huyo.
Pamoja na
kuandika barua hiyo iliyopokewa na mahakama, ilibainika kuwa na
upungufu wa kisheria na kutakiwa kuifanyia marekebisho.
Lakini
ghafla mtuhumiwa huyo alipotolewa mahakamani na kuingizwa kwenye gari la
polisi, alivamiwa na walalamikaji hao na kuanza kumshambulia.
Baada ya
kuona walemavu hao wa ngozi wamewazidi nguvu, askari waliamua kuondoa
gari na kuelekea katika kituo cha Buguruni, ambako waliomba msaada na
baada ya muda waliwanya kwa mabomu ya machozi.
Akizungumzia
kuhusu hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Albino Wilaya ya Temeke, Kasim
Kibwe, alisema suala la kuwalinda ni dhahiri Serikali imeshindwa, hivyo
kuomba msaada kutoka nje ya nchi.
Alisema
hatua hiyo itawasaidia kulindwa wakati wote, kwani matukio ya watu wenye
ulemavu wa ngozi yamekuwa wakiongezeka kila siku.
"Inasikitisha
kuona hapa nchini wanyamapori wanalindwa kwa nguvu kubwa kuliko sisi
albino ambao ni binadamu, hali inayonifanya nifikirie kuwa mkimbizi nje
ya nchi kuliko kuwa raia hapa nchini. Na hivi kuna uhusiano gani wa
kuuawa kwa albino inapokaribia kipindi cha uchaguzi mkuu?" alisema
Kibwe.
Kwa
upande wake, Mwekahazina wa Chama cha Maalbino Taifa, Abdillah Omary,
aliwataka albino wenzake kuwa watulivu katika kesi hiyo.
Kamanda
wa Polisi Wilaya ya Ilala, Mary Nzuki, alithibitisha kutokea kwa vurugu
hizo, huku akisema kuwa hali hiyo imechangiwa na mwili wa mwanamume
mmoja aliyedhaniwa ni mlemavu wa ngozi kuokotwa amefariki dunia Tabata
Kinyerezi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kamanda
Nzuki alisema mwili huo kwa sasa upo katika uchunguzi unaowajumuisha
viongozi wa Chama cha Albino Tanzania pamoja na wawakilishi wa Shirika
la Under The Same Sun kubaini ukweli, na taarifa baada ya kukamilika
zitatolewa wiki ijayo.
Alisema
kuwa wakati wa tukio hilo, mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Mwenyeusi
Issa (39), alidai kumsikia mtuhumiwa, Ombeni Michael (34) akitoa kauli
ya kutishia kuwaua albino, huku akiwa anakunywa pombe baa.
0 comments:
Post a Comment