Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma imebarikiwa kuwa na fukwe za asili ambazo hazifanani na fukwe nyingine zozote duniani.
Ikiwa fukwe hizi zitaendelezwa zinaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato katika wilaya mpya ya Nyasa.
Jambo la kusitikisha ni kwamba licha ya mwambao wa
ziwa Nyasa kubainika kuwa na fukwe bora duniani ambazo zinaweza
kufungua utalii katika ziwa Nyasa, kwa upande wa Tanzania hadi sasa
bado hakujawa na juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa fukwe zilizopo
zinaibuliwa na kuwa chanzo cha mapato.
Fukwe ya Bayi
Hata hivyo, fukwe ya Bayi iliyopo katika eneo la
Ndengere kata ya Mbambabay wilayani Nyasa, imeanza kuendelezwa na
mwekezaji binafsi ambaye tayari ameanzisha vivutio mbalimbali vya utalii
kuvutia watalii wengi wa ndani na nje ya nchi .
Moja ya mambo ambayo yameipandisha chati fukwe ya
Bayi ni pale mwekezaji alipoamua kuanzisha utalii wa michezo ambapo hivi
sasa kuna mchezo unaoitwa ndege kidogo.
Raia mmoja wa kigeni ndiye anayefundisha wazalendo
kucheza mchezo huo wa ndege ambao unapendwa na watu wengi kuangalia
ndege hiyo inaporuka juu katika fukwe hiyo.
Ndege ina uwezo wa kubeba mtu mmoja ambayo
inaruka juu kwa kusaidiwa na parachuti umbali wa meta 60 na kusafiri
umbali wa kilometa 80 kwa saa
Utalii wa ndege kidogo unavutia wakazi wengi wa
mwambao mwa ziwa Nyasa ambao wanatembelea fukwe ya Bayi kila siku kwa
lengo la kushiriki katika aina hiyo mpya ya utalii iliyoanzishwa katika
ziwa Nyasa.
Raia wa nchini Marekani ambaye ndiye
aliyetengeneza ndege ndogo anasema ndege hiyo ina uwezo wa kubeba mtu
mmoja ambaye anaruka akiwa amesimama huku mwili wake ukiwa nje.
Ndege hiyo inatumia mafuta kidogo kwenye galoni la
lita tano ambayo yanabebwa mgongoni, mchezaji wa mchezo huo kichwani
anakuwa amevaa kofia maalumu inayomkinga na upepo akiwa angani.
Meneja wa Fukwe ya Bayi Joseph Chengula anasema
ukiachia utalii wa mchezo wa ndege kidogo, mtu anayetembelea fukwe hiyo
katika eneo hilo anaweza kufanya utalii katika ziwa Nyasa kwa kuangalia
fukwe ya Bayi ambayo inaongoza kwa ubora katika ziwa Nyasa na kwamba
mtalii pia anaweza kufanya utalii kwa kusafiri katika boti ndani ya ziwa
na kuona vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya ziwa hilo.
0 comments:
Post a Comment