Thursday, 7 August 2014


Katika jitihada za kuliepusha Bunge la Katiba kupoteza mwelekeo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wajumbe wake kuacha kumjadili mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliosusia vikao vya Bunge hilo.
Badala yake, CCM imewaelekeza wajumbe hao kujadili “mambo yanayowahusu wananchi” ambayo yamependekezwa katika Rasimu ya Katiba.
Maelekezo hayo yalitolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipokutana na wajumbe wa Bunge Maalumu ambao ni wabunge wa Jamhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wale walioteuliwa kuingia katika Bunge hilo kupitia wajumbe wa kuteuliwa na Rais kupitia kundi la 201.
Kikao hicho ambacho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa CCM Makao Makuu, pamoja na mambo mengine pia kiligusia mwenendo wa Bunge la Katiba, huku Kinana akitoa maelezo mafupi kuwahakikishia msimamo wa chama hicho kwamba kinaunga mkono hatua za kuendelea kwake katika awamu ya pili.
Maelekezo hayo yamekuja baada ya wajumbe hao kutumia muda mwingi wa siku ya kwanza ya awamu ya pili ya Bunge la Katiba, kuwashutumu wajumbe wa Ukawa kwa kususia vikao, wakiwaeleza kuwa mwafaka unaweza tu kupatikana ndani ya chombo hicho cha kuandika katiba.
Wajumbe hao walidiriki hata kutafuta mfumo wa kuwazuia wajumbe hao wa Ukawa kuzungumzia Katiba wakiwa nje ya Bunge Maalumu.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho ambazo gazeti hili lilizipata zinasema wajumbe hao walimwomba Kinana kuwa Ukawa na Jaji Warioba wazuiwe kujadili Katiba nje ya Bunge.
Kinana, akijibu hoja hiyo katika kikao hicho kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema wajumbe hao wa CCM hawapaswi kulumbana na watu walioko nje ya Bunge na asingependa kusikia wakiwataja Ukawa wala Warioba wakati wakichangia bungeni.
Kadhalika Kinana alisema chama hicho hakiwezi kushawishi kuzuiwa kwa mikutano wala mijadala inayoendeshwa nje ya Bunge Maalumu la Katiba.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa suala hilo la wajumbe wa Ukawa na Jaji Warioba lilitawala mjadala kwa dakika kadhaa kutokana na baadhi ya wajumbe kupinga mawazo ya kukaa kimya, lakini Kinana aliwaambia kwamba kama wanataka kujibizana na Ukawa au watu wanaozungumza kwenye midahalo, iwe maeneo mengine, akisema Bunge si mahali pake.
“Alisema kama tunataka kuwajibu Ukawa na wengine, basi tuandae midahalo au mikutano ya hadhara na kwamba bungeni ni mahali pa kujadili mambo muhimu tena siyo yanayohusu watawala, bali yanayowahusu wananchi,” kilisema chanzo chetu kikimkariri Kinana.

0 comments:

Post a Comment