Friday, 15 August 2014

Rais Jakaya Kikwete amesema suala la uraia wa nchi mbili linaonekana kutokuwa na nguvu kwa sasa kutokana na kutojitokeza katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hivyo kutoingia katika Rasimu ya Katiba inayojadiliwa sasa bungeni.
Kauli ya Rais Kikwete imekuja wakati suala hilo likionekana kuwagawa wajumbe katika Kamati za Bunge Maalumu, kutokana na kuwapo kwa mapendekezo kwamba suala uraia pacha liingizwe kwenye rasimu hata kama halikuwekwa na Tume.
Juzi, suala hilo liliwagawa wajumbe wa Kamati Namba mbili inayoongozwa na Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na kusababisha ibara hiyo kukosa theluthi mbili ya kura kutoka pande zote za muungano.
Akizungumza katika kongamano maalumu linalowakutanisha Watanzania waishio nje ya nchi Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema suala hilo limekosa wasemaji wanaoguswa moja kwa moja ambao wangeweza kulitetea, hivyo kutokuwa miongoni mwa vipaumbele katika rasimu hiyo.
“Msijipe matumaini kwa sababu kwa namna ilivyoandikwa kwenye Rasimu ya Katiba, haiwezi kuzaa uraia wa nchi mbili, bali inaweza kutoa stahiki ya fursa wanazoweza kupata Watanzania waishio nje ya nchi, kupitia sheria,” alisema.
Kongamano hilo la kwanza la siku mbili linawakutanisha Watanzania waishio katika nchi 17 duniani, lililoandaliwa na Asasi ya Tanzania Diaspora Initiative (TDI).
Rais Kikwete alisema Serikali yake inafahamu umuhimu wa kupatikana kwa uraia pacha kwa watu wake lakini suala la uraia ni la kikatiba na siyo la Rais kwa kuwa Katiba ndiyo inayoamua.
Alisema hata chama chake (CCM), kilipojaribu kuliingiza lilionekana kutokuwa na nguvu ya kutosha kwa kuwa hakuna ambaye lilikuwa likimgusa moja kwa moja.
Aliwashauri kuwatumia wajumbe katika Bunge linaloendelea mjini Dodoma ili wapaze sauti zao na ikiwezekana watumie fursa zote za mawasiliano kufikisha ujumbe wao.
“Sisi upande wa Serikali tunaliona ni suala jema, ila halina nguvu kwa sababu wabunge wengi haliwagusi moja kwa moja, hivyo si rahisi kulipigania. Mbona nchi nyingine watu wao wananufaika na hili! Kwa nini hapa kwetu lishindikane?” alihoji.
Ndani ya kamati
Habari kutoka ndani ya kamati zinasema wajumbe wamegawanyika kuhusu suala hilo na wengine wameshindwa kufikia mwafaka kama ilivyotokea katika Kamati namba 11 inayoongozwa na Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela.

0 comments:

Post a Comment