mahindi yaliyohifadhiwa na hifadhi ya chakula mkoa wa ruvuma.
BAADHI ya Wasafirishaji wa mazao ya nafaka mkoani Ruvuma, wameiomba
Serikali kuangalia uwezekano wa kuharakisha kulipa madeni yao ya usafirishaji
wa mahindi kutoka kwenye vituo vya ununuzi na kuyafikisha kwenye kitengo cha
hifadhi ya chakula (NFRA) Songea mkoani humo, katika msimu wa kilimo wa mwaka
2013/2014 kwa lengo la kunusuru kuuziwa mali zao na taasisi za kifedha ambako
walikopa kwa ajili ya kuendeshea shughuli hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasafirishaji
hao ambao ni wazawa hawakutaka majina yao yatajwe, walidai kwamba hali hiyo
imewaathiri zaidi waajiriwa waliopitia
mgongo wa nyuma kufanya kazi ya usafirishaji wa zao hilo baada ya matajiri wao
kuingia mkataba na NFRA.
Walisema kuwa tangu kufunguliwa kwa msimu huo Julai 15 mwaka
jana wamekuwa wakiendesha shughuli hizo kwa kutegemea mikopo kutoka benki, na
wengine kudaiwa na baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta ambako walikopa.
Walieleza kuwa endapo serikali haitalifanyia ufumbuzi wa
haraka suala hilo shughuli ya usafirishaji wa mahindi kutoka katika vituo mbalimbali
katika msimu wa mwaka huu, kuna uwezekano wa kazi hiyo kuwa ngumu kutokana na
wasafirishaji hao kukosa mitaji ya kuendeshea kazi hiyo.
“Sisi tuna nia nzuri ya kufanya biashara na serikali yetu, katika
kuhakikisha tunasafirisha mahindi toka kwenye vituo huko vijijini ambako miundo
mbinu yake ya barabara sio mizuri na kuyapeleka kwenye kitengo cha hifadhi ya
chakula Songea”,
“Lakini magari yetu yamekuwa yakiharibika mara kwa mara
wakati tunafanya kazi hii, tunaiomba serikali iangalie uwezekano wa kutulipa
mapema madeni tunayoidai ili magari yaweze kufanyiwa matengenezo na kulipa
madeni tunayodaiwa ambako tulikopa”, walisema.
Kwa upande wake Meneja wa kanda kitengo cha hifadhi ya
chakula (NFRA) Songea mkoani Ruvuma, Morgan Mwaipyana alikiri kuwepo kwa madai hayo huku akieleza kuwa serikali
ipo mbioni kuhakikisha Wasafirishaji hao wanalipwa fedha zao mara baada ya
taratibu husika kukamilika.
Mwaipyana alifafanua kuwa NFRA mpaka sasa haidaiwi na mtu
yeyote zaidi ya wasafirishaji wa mazao kwa kuwa Serikali katika msimu wa mwaka
2013/2014 imeweza kulipa madeni ya wakulima na mawakala wote ambao waliuza
mahindi yao katika kitengo hicho cha hifadhi ya chakula kilichopo mjini hapa.
Wadai hao walifanya kazi ya kusafirisha mahindi hayo kutoka maeneo mbalimbali ambayo vituo vya
ununuzi vilitengwa katika wilaya ya
Songea, Mbinga na Namtumbo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2013/2014.
0 comments:
Post a Comment