“Kila siku naomba Mwenyezi Mungu anichukue
haraka ili nikapumzike kutokana na mateso ninayoyapata, lakini hofu
yangu nikifa je, nitazikwa kama binadamu wengine? Ndiyo maana nimeamua
kujitayarishia jeneza langu,” anasema Scholastica Mhagama (76) mwenye
ulemavu wa viungo anayeishi pekee yake katika kibanda kilichoezekwa kwa
nyasi.
Bibi huyo mkazi wa Kijiji cha Lundusi Kata ya
Peramiho wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma, anasema kwa miaka mingi ameishi
katika kibanda hicho alichojengewa na mzungu aliyemtaja kwa jina moja
la Kilibada ambaye pia anasema alikuwa akimsaidia kulima mihogo.
Anaongeza kuwa maisha yake yanategemea kukaa nje
ya kibanda chake na kuomba msaada kwa watoto wanaopita ambao huwaomba
wamchotee maji.
Anabainisha kuwa mara chache anaweza kutokea mtoto
ambaye humchotea maji kwenye ndoo ndogo ya lita kumi ambayo huyatumia
kwa matumizi ya kuoga, kupikia, kunywa na kwamba hayatoshi kufulia wala
kufanya kazi nyingine hali ambayo inamsababishia kuvaa nguo chafu wakati
wote.
Anasimulia kuwa huwa anapika mara chache ndani ya
kibanda anacholala na hata sehemu anayolala haina kitanda, godoro wala
mkeka badala yake amekuwa analala chini katika mfuko wa mbolea na
kujifunika blanketi kuu kuu.
“Ona kwanza mwanangu mahali ninapolala hakuna
kitanda wala mkeka, mifuko ambayo ndiyo godoro langu huwa ninaomba tu.
Nahitaji msaada, sina uwezo wa kufanya kazi yoyote tangu nilipokatwa
mguu wa kulia nilipokuwa darasa la tatu hadi sasa nimekuwa naishi kwa
shida ingawa sasa katika uzee hali imekuwa mbaya zaidi,’’ anasema.
Ajitengenezea jeneza
Kutokana na kushindwa kupata msaada kutoka kwa
ndugu na majirani zake, Scholastica ameamua kutengeneza jeneza lake
kabla ya kufa akihofia kuzikwa katika mkeka kwa kuwa ameshindwa
kusaidiwa akiwa hai, hivyo anaamini akifa anaweza kutupwa kama mzoga wa
mnyama asiye na faida yoyote.
“Nimetengeneza kabisa jeneza langu siku nikifa
wanizike humu. Naomba Mungu anichukue haraka ili kuepukana na mateso
haya. Nimetengwa na jamii na majirani wanashindwa kunisaidia wanadai eti
mimi ni mchawi kwa sababu watoto wangu wote wanne walikufa wakiwa
wadogo. Naumia sana kusingiziwa kitu ambacho sikijui,’’ anasema kwa
masikitiko.
Bibi huyo anasema kuwa aliweza kutengeza jeneza hilo baada ya kupewa Sh40,000 na mfadhili mmoja.
“Tayari nilikuwa na mbao kwangu, hivyo kazi ilikuwa kumlipa kijana fedha na kumpa mbao ili anitengenezee jeneza,” anasema.
Hata hivyo, aliitaja misaada ya haraka ambayo
anahitaji ili aweze kuishi kuwa ni pamoja na baiskeli ya miguu mitatu
(wheel chair) ambayo itamwezesha kutembea kwa kuwa hivi sasa amekuwa
anatambaa na kupata maumivu makali kutokana na nyama iliyobakia kwenye
nyonga baada ya kukatwa mguu.
0 comments:
Post a Comment