Tuesday, 12 August 2014

Mjadala kuhusu masuala ya Muungano unatarajiwa kurejea upya katika kamati za Bunge Maalumu leo, wakati zitakapoanza kujadili sura za saba, nane, kumi na moja, 18 na 15 za Rasimu ya Katiba.
Kamati zimepewa siku sita kujadili sura hizo tano ambazo zina jumla ya ibara 79, huku miongoni mwake zikigusa masuala mengi ambayo msingi wake umejengwa juu ya mfumo wa serikali tatu.
Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na baraza la mawaziri, tume ya kusimamia na kuratibu uhusiano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali za Nchi Washirika (Tanganyika na Zanzibar), Sekretarieti ya Tume ya Uhusiano na Uratibu, Masuala yanayohusu Benki Kuu na Fedha pamoja na uteuzi wa watumishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Suala la aina ya muungano lilianza kujadiliwa katika sura ya kwanza na ya sita katika awamu ya kwanza ya Bunge iliyomalizika mwishoni mwa Aprili mwaka huu na kuzua mvutano mkali ambao hatimaye ulisababisha baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kususia mchakato huo.
Wajumbe hao ni wale wanaotokana na vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao wanataka mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ya kuwapo kwa muundo wa serikali tatu yabaki kama yalivyo na upande mwingine unaowajumuisha wabunge wengi wa CCM ukitaka muundo wa sasa wa Serikali mbili uendelee.
Kutokana na mvutano huo, Bunge Maalumu liliahirisha upigaji kura kuamua aina ya muundo unaofaa, lakini hata liliporejea Agosti 5, mwaka huu halikuweza kupiga kura, badala yake lilibadilisha kanuni ili kuwezesha upigaji kura kufanyika baada ya kumaliza mjadala wa sura zote ndani ya kamati. 
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hakuna maelekezo yoyote yaliyotolewa kwa wajumbe kuhusu jinsi ya kujadili masuala yanayohusu muungano na kwamba wajumbe watazingatia mapendekezo waliyoyatoa katika rasimu ya kwanza na ya sita.
“Sidhani kama ni wajibu wetu kutoa maelekezo yoyote, kinachoweza kutokea ni wajumbe kuzingatia kila walichokijadili na kukubaliana katika sura zile za awali, kama walikubali serikali ya shirikisho watazingatia hilo, kama walikubaliana serikali mbili watazingatia hilo pia,” alisema Hamad.
Itakumbukwa kwamba idadi kubwa ya kamati baada ya kujadili sura ya kwanza na ya sita zinazohusu aina ya muungano, zilipendekeza kuachana na muundo wa shirikisho na kuwasilisha maoni yanayotaka kuendelea kwa mfumo wa Serikali mbili. Kamati nyingi zilipata idadi ya kura za kutosha kuunga mkono mapendekezo hayo na chache zilikosa theluthi mbili kutoka kwa wajumbe wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Ikiwa kamati hizo zitazingatia uamuzi wake wa awali, basi masuala yote yanayogusa serikali tatu yatafutwa, hivyo zitakuwa na kazi kubwa ya kuandika upya ibara nyingi zinazozingatia utekelezaji wa mfumo serikali mbili.
Maudhui ya Ibara
Ibara ya 98 ya Rasimu pamoja na mambo mengine, inazungumzia idadi ya mawaziri ambao idadi yao hawapaswi kuzidi 15, huku uteuzi wao ukipendekezwa uthibitishwe na Bunge.

0 comments:

Post a Comment