Sunday 20 July 2014



CHIPUKIZI Omar Wayne juzi alionyesha ni hazina nzuri ya taifa, baada ya kucheza vizuri mno katika nafasi ya kiungo, timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ikilazimishwa sare ya bila kufungana na Afrika Kusini, Amajimbos.
Katika mchezo huo wa kwanza wa Raundi ya Pili kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika nchini Nigeri mwakani, uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Wayne alicheza nafasi ya kiungo wa katikati.
Kiungo hodari wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ni miongoni mwa waliokunwa na vitu vya kinda huyo na akasema; “Yule mtoto mwenye jezi namba nane kaitendea haki ile nafasi, ni kiungo bora kabisa wa baadaye,”.
Omar Wayne akimtoka Nahodha wa Amajimbos, Nelson Malukele
Sure Boy alivutiwa na vitu vya Omar Wayne juzi Chamazi
Wayne alivutia wengi miongoni mwa watazamaji waliokuwepo uwanjani kwa soka yake- kutokana na kucheza kwa ubora kwenye nafasi ya kiungo, ambayo ni roho ya timu.
Alisaidia ulinzi, aliisafirisha timu vizuri kwenda kwenye ngome ya wapinzani, akitoa pasi maridadi na za uhakika. Alitafuta mipira, alikaba. Alikuwa anapasua kuisogeza timu juu katika kutengeneza shambulizi. Ilipobidi yeye mwenyewe kupandisha mpira, alifanya hivyo.
Omar Wayne akiwafunga tela Amajimbos
Omar Wayne anakaba
Omar Wayne anasafiri katikati ya msitu wa Aamajimbos

Uwezo mzuri wa kumiliki mpira, maarifa ya kisoka kiasi cha kujua wakati gani afanye nini- vyote vinamaanisha Wayne ni tegemeo la Tanzania baadaye.
Kipaji chake kinahitaji kumulikwa na kupatiwa malezi mazuri ya kisoka, ili ndoto zake zitimie. Wayne ni mchezaji ambaye wasaka vipaji wa klabu kubwa Ulaya wakimuona hata sasa watampenda na kumpigia hesabu. Hawezi kuendelezwa hapa Tanzania, huyu ni aina ya vijana ambao wanatakiwa wapelekwe katika akademi za klabu za Ulaya, ili siku moja Tanzania ije kujivunia wachezaji wanaocheza klabu kubwa duniani.
Matokeo ya sare na Amajimbos, yanamaanisha, Serengeti Boys itahitaji sare ya mabao katika mchezo wa ugenini, au kushinda kabisa ili kuingia hatua ya mwisho ya mchujo katika kuwania tiketi ya Fainali zitakazopigwa Niger mwakani.
Iwapo Tanzania itatolewa, bado TFF itakua na wajibu wa kuutazama mustakabali wa vijana waliokuwa wanaunda Serengeti Boys- juu ya namna ya kuwandeleza.
Wakiendelezwa vizuri, ni miaka minne ijayo tu watakuwa tayari kulibeba taifa. Dogo kama Omar Wayne, miaka mitatu ijayo anaweza kuwa mchezaji wa klabu kubwa Ulaya. Ni mipango tu. 

0 comments:

Post a Comment