Rais wa Marekani, Barack Obama amesema Afrika inahitaji viongozi vijana katika nyakati hizi, kwa kuwa ndiyo wenye uwezo wa kujenga uhuru, kujitegemea na usimamizi mzuri wa haki za raia na utawala wa sheria.
Kauli hiyo ya Obama imekuja ikiwa ni siku chache tangu baadhi vijana nchini kutangaza kuwania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Vijana hao ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Kujitangaza kwao kuliibua maoni tofauti kwa wananchi huku wengine wakipinga na wengine kukubali uamuzi wao.
Akizungumza na viongozi vijana, wanafunzi na wanaharakati zaidi ya 500 waliokusanyika mjini Washington kama sehemu ya utangulizi wa mkutano huo wa wakuu wa nchi, Obama alisisitiza kwamba Afrika inahitaji viongozi vijana wanaojali umuhimu wa demokrasia, kwa kuwa wana uwezo wa kuangalia mahitaji ya sasa na ya kizazi kijacho kwa uhakika.
“Ulinzi, uwezo na haki tunayotafuta duniani haviwezi kupatikana bila kuwa na Afrika imara yenye uwezo na inayojitegemea,” Obama aliwaeleza zaidi ya vijana 500 waliokusanyika mjini Washington.
“Wiki ijayo nitaongoza tukio moja kubwa la kihistoria, ambalo ni la mkutano wa viongozi wa nchi 50 za Afrika, litakuwa ni kubwa kuwahi kufanywa na Rais wa Marekani na wakuu wa nchi za Afrika katika historia,” aliongeza.
Mkutano huo hautawahusisha viongozi wa Afrika ambao wamekaa muda mrefu madarakani, miongoni mwao ni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Omar al-Bashir wa Sudan na Issaias Afeworki wa Eritrea. Mkutano huo unafanyika wakati Shirika la Fedha Duniani (IMF) likieleza kwamba uchumi wa nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara utakua kwa asilimia 5.4 mwaka huu na asilimia 5.8 mwakani, ikiwa ni ongezeko la kasi kidunia.
Marekani inaendelea kuwa taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani, huku Afrika akiwa mshirika wake wa tatu kibiashara baada ya Umoja wa Ulaya (EU) ambao baadhi ya nchi washirika zimekuwa na historia ya kuitawala enzi za ukoloni na China, ambayo pia imekuwa na kiu kubwa ya kuvuna rasilimali zilizopo Afrika.
Obama ambaye baba yake ni mzaliwa wa Kenya na mama yake mzaliwa wa Marekani, amekuwa rais wa kwanza mwenye asili ya Afrika nchini Marekani na mara kadhaa amekuwa akilaumiwa kwa kutojenga uhusiano mzuri na Afrika.
0 comments:
Post a Comment