Friday 1 August 2014

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umesema licha ya viongozi wa dini kuwataka warejee katika Bunge Maalum la Katiba, hawatafanya hivyo kwakuwa wameonyesha upendeleo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, wamesema wanawaheshimu viongozi wa dini, lakini wamesikitishwa na matamko yao yaliyoshindwa kukemea matendo ya viongozi wa CCM, isipokuwa wamekuwa wakiwataka UKAWA warejee bungeni.

Kauli hiyo ya UKAWA inakuja siku chache baada ya viongozi wa dini wakiwa kwenye Baraza la Idd, kuwataka warejee katika Bunge la Katiba linalotarajia kuanza Agosti 5.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema licha ya heshima yao kwa viongozi wa dini, lakini wamekuwa wakisikitishwa na baadhi ya matamshi yao kana kwamba hawajui kilichowaondoa bungeni katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Lipumba alisema sababu zilizowafanya UKAWA kutoka nje ya Bunge ni kutokubali mkakati wa wajumbe kutoka CCM wa kupuuza maoni ya wananchi yaliyokusanywa na kuratibiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Alisema rasimu ya katiba inapendekeza muundo wa muungano wa shirikisho lenye serikali tatu, lakini wajumbe wengi wa CCM wameng’ang’ania serikali mbili na kuamua kubadilisha kanuni za Bunge Maalum kuruhusu matakwa yao.

“Muundo wa muungano ndiyo moyo wa rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi, CCM wameukataa muundo wa muungano uliopendekezwa na tume na badala yake wanataka muundo wa serikali mbili ambao haujafanyiwa utafiti, haujapendekezwa na wananchi walio wengi, uliojaa matatizo lukuki yasiyotatulika tangu enzi za uhuru na ambao haujapendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema.

Lipumba alisema sababu nyingine iliyowaondoa bungeni ni kukwazwa na lugha za ubaguzi, uchochezi, matusi na kejeli zilizokuwa zikiporomoshwa na baadhi ya wajumbe wa CCM ndani na nje ya Bunge la Katiba.

Michango mingi ya wajumbe wa CCM katika Bunge Maalum ilikuwa ya kumkejeli na kumdhalilisha Jaji Joseph Warioba na kauli za kibaguzi dhidi ya Waarabu, Wapemba na Wahindi.

“Lugha kama hizo za kibaguzi na kichochezi pia zilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alipokuwa anamuwakilisha Waziri Mkuu Pinda katika ibada ya kumsimika Askofu wa Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma  ambapo aliwataka wananchi waliohudhuria ibada hiyo kupinga serikali tatu  zilizopendekezwa  na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi hao, lakini hajachukuliwa hatua zozote hadi leo wala kuonywa.

“Ninyi ni mashahidi jinsi wajumbe wa CCM walivyoporomosha matusi makubwa na tuhuma nzito dhidi ya Jaji Warioba, baadhi ya wajumbe waliwaita wajumbe wa tume hii kuwa wasaliti wa baba wa taifa, wazee wanaosubiri kufa na watu wasiokuwa na uzalendo bali wana ajenda binafsi,” alisema Lipumba.

Alieleza sababu nyingine iliyowafanya kutoka bungeni ni kutokana na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kuvunja kanuni kwa kumtanguliza mwenyekiti wa tume kuwasilisha rasimu kabla Bunge kusikiliza hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi, na kwamba ametishia kufanya hivyo tena kwa sasa.

Lipumba alisema wameondoka bungeni kutokana na Sitta kushindwa kuwadhibiti wajumbe wanaotumia lugha za kibaguzi, uchochezi, matusi na kwamba baadhi ya kauli walizikabili ndani ya Bunge na kuwaonya CCM kuacha badala yake watumie jukwaa hilo kusaidia upatikanaji wa katiba na hawakusikilizwa.

Alisema kutokana na vitendo vyote hivyo wanavyofanyiwa, walitegemea pia viongozi wa dini hao wanaokutana na serikali na chama tawala na kufanya mazungumzo nao wangewahusisha na wao ukawa.

“Miito ya viongozi hao wa dini inaelekeza upande mmoja ikifumbia macho upande wa pili, na kwamba sisi tunaamini viongozi wetu wa kiroho wana uwezo wa kuangalia pande zote mbili na kutoa miito yenye ukweli, usawa na haki, hivyo tunawasihi kabla ya kututaka kurejea bungeni wangetumia busara hiyo kutusikiliza na sisi kama ambavyo wanawasikiliza viongozi wa CCM,” alisema Lipumba.

Kauli ya Mbowe


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) akijibu swali aliloulizwa na mmoja wa waandishi wa habari kama watarejea bungeni baada ya kuona tangazo la kuanza kwa vikao hivyo wiki ijayo, alisema kama kutakuwa na miujiza ya CCM kujirekebisha na kutenda haki, watafanya hivyo.

Alisema anashangazwa katika mazingira ya sasa ambapo viongozi wa juu wa UKAWA na CCM wakiwa katika mazungumzo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Sitta, anatoa matamko na tishio la kuwadhibiti zaidi iwapo hawataenda bungeni.

“Sisi tupo katika mazungumzo, na bosi wake Waziri Mkuu Pinda, anatoa matamko yake, Sitta naye anatoa matamko yake kiasi cha kwamba hakuna muungano na kila mtu amekuwa akijisemea kwa upande wake, sasa kwa hali hii tunaweza kusema hawa wapo pamoja? Hatuwezi kurejea kama wataendelea hivi,” alisema Mbowe.

Pia akijibu swali aliloulizwa kama watahudhuria mkutano wa leo utakaowakutanisha baadhi ya wanasiasa wa makundi mbalimbali, alisema watashiriki, na mkutano huo ndiyo utakaotoa majaliwa ya wao kushiriki vikao vya Bunge Maalum.

“Kikao cha kesho nacho kitaamua majaliwa yetu, ngoja tuone matokeo ya mazungumzo… kama wakikubaliana na hoja zetu tunaweza kufanya maamuzi mengine,”  alisema.

Kauli ya Mbatia


Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, alisema hawawezi kuliendesha taifa bila kuwa na uadilifu, utu, uzalendo na kuangalia kule linakoelekea.

Alijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua kama watashiriki uchaguzi mkuu bila katiba, alisema kuna mambo mengi yanayohitaji kufanyiwa kazi, ikiwemo kubadilisha sheria za uchaguzi, tume huru ya uchaguzi ambavyo vyote vinajengwa na msingi mkuu ambao ni katiba.

0 comments:

Post a Comment