Askofu wa Kanisa la Christian Fellowship Assemblies of God la Arusha,
Jumanne Kilongola amehukumiwa kifungo cha miaka 32 jela baada ya
kupatikana na hatia ya kupora Sh5.3 bilioni ndani ya Benki ya NBC, Tawi
la Moshi Mei 21, 2004.
Katika
hukumu hiyo iliyotolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kilimanjaro, Simon Kobelo, askofu huyo amehukumiwa kifungo
hicho pamoja na raia watano wa Kenya baada ya kupatikana na hatia ya
kufanya wizi huo kwa mtutu wa bunduki.
Kati
ya fedha hizo, Sh126.2 milioni zilikuwa mali ya Benki ya NBC wakati
Sh5.1 bilioni ni mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ilikuwa
ikitumia NBC Moshi kama kituo chake kidogo.
Ilielezwa
mahakamani hapo wakati wa ushahidi kuwa Askofu Kilongola ndiye
aliyekodi gari aina ya Toyota Landcruiser lililotumiwa kubeba fedha hizo
kwa Sh320,000 na alimweleza mmiliki wake kuwa alikuwa anakwenda kubeba
wanakwaya wake.
Raia
wa Kenya waliohukumiwa kifungo hicho cha miaka 32 ni Wilfred Onyango
Nganyi, Patrick Muthee Murithi, Gabriel Kungu Kariuki, Jimmy Maina
Njoroge na Simon Ndungu Kiambuthi.
Hata
hivyo, mahakama hiyo iliwaachia huru raia wengine watatu wa Kenya,
Boniface Mwangi Mburu, David Ngugi Mburu na Michael Mbanya Wathigo
kutokana na kukosekana ushahidi dhidi yao.
Hakimu
Kobelo alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali,
Hyra Sande, Ladslaus Komanya na Stella Majaliwa umethibitisha pasipo
shaka kuwa washtakiwa hao waliohukumiwa walitenda makosa hayo.
Alisema
ushahidi dhidi ya Askofu Kilongola na raia hao wa Kenya ulikuwa
madhubuti kutokana na kutambuliwa kikamilifu na mashahidi katika gwaride
la utambuzi.
Hakimu
huyo alisema Mahakama imewahukumu kifungo cha miaka 30 kwa unyang’anyi
wa kutumia silaha na miaka mingine miwili kwa kosa la kula njama ya
kupora fedha hizo.
Hakimu
Kobelo aliamuru Dola za Marekani 39,000, sawa na Sh64 milioni
walizokutwa nazo washtakiwa zitaifishwe na Serikali na zikabidhiwe kwa
uongozi wa Benki ya NBC. Hukumu hiyo imekuja wakati jitihada za Tanzania
kuwarejesha nchini, wahalifu watatu kutoka Kenya na Uganda, wanaodaiwa
kuvamia benki hiyo zikiwa zimegonga mwamba.
Watuhumiwa
hao ni Patrick Ayis Ingoi, raia wa Kenya anayedaiwa kuwa kiongozi wa
genge la majambazi hao, Charles Lumago na Shaban Wayabona ambao ni raia
wa Uganda.
Hukumu
hiyo inafanya idadi ya waliofungwa kwa uporaji huo kufikia 12, baada ya
Watanzania wanne kufungwa kwa kosa hilohilo Desemba 13, mwaka 2006.
Watanzania
hao ni Jackson Ole Nametemi, Benjamin Dia, Kelvin Dia na Raphael
Kalaghe waliofungwa miaka 30 na Evelyne Mlaki na Happy Memei waliofungwa
miaka mitatu.
Mlaki
na Memei walitumikia vifungo vyao na kumaliza wakati washtakiwa wengine
walikata rufaa Mahakama Kuu na hukumu yake haijatolewa kwa miaka mitano
sasa.
|
0 comments:
Post a Comment