Saturday 30 May 2015


Mbio za urais zimezidi kupamba moto kwa upande wa upinzani baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo ya juu kisiasa nchini, akisema ana sifa zote lakini hatakuwa na kinyongo iwapo hatapitishwa na umoja wa vyama vya upinzani.
Profesa Lipumba, ambaye anakuwa mwanasiasa wa tatu kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza nia hiyo baada ya mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi na Dk George Kahangwa wa NCCR-Mageuzi kujitokeza kutaka kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwanasiasa mwingine aliyejitokeza kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano ni Maxmillan Lyimbo wa TLP, wakati Hamad Rashid wa Alliance for Democratic Change (ADC na Maalim Sharrif Hamad wa CUF wametangaza kuwania urais wa Zanzibar.
Lipumba, ambaye atakuwa akiwania urais kwa mara ya tano, iwapo atapitishwa na Ukawa ambayo imeamua kusimamia mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vinne, alitangaza nia yake juzi mjini Tabora wakati wa mikutano yake ya hadhara ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
“Ninachoomba ni ushirikiano wenu katika safari yangu hii ya kuwania tena urais,” alisema Profesa Lipumba alipokuwa akihutubia wananchi kwenye uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi ya Town School mjini hapa.
“Ninajua safari hii, urais (kwa upande wa upinzani) utasimamiwa na Ukawa, lakini naamini mimi ni mwadilifu na nina uwezo wa kuongoza nchi,” alisema Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba aliwaomba wapenzi na wanachama wa CUF pamoja na Watanzania kwa ujumla, kumuunga mkono katika safari yake hiyo ya kuelekea Ikulu.
Mwenyekiti huyo wa CUF ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema ana uwezo na sifa za kuwa rais na kwamba madhumuni makuu ya kutaka kushika madaraka ni kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi na kupambana na ufisadi.
“Dhumuni kuu si cheo, bali ni kushirikiana na wananchi kuondoa kero zao,” alisema mshauri huyo wa zamani wa uchumi wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.
Lakini alikuwa makini na azimio la umoja huo wa wapinzani unaoundwa na CUF, NLD, NCCR-Mageuzi na Chadema, kuhusu kusimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama hivyo.
“Ingawa Ukawa itakuwa na mgombea mmoja wa urais, naamini kuwa mimi ni miongoni mwa wanaofaa kupeperusha bendera hiyo kwa kuwa najijua kuwa ni mwadilifu na nina uwezo wa kuliongoza Taifa changa kiuchumi kama Tanzania,” alisema Profesa.
“Mimi naweka nia ya kugombea urais nikiwa na malengo mengi, ikiwamo kutaka kumaliza kero ya umaskini kwa Watanzania, lakini kikubwa ni ushirikiano wenu katika safari hii.

0 comments:

Post a Comment