Askofu mkuu Damian Dallu wakati akitoa mahubiri katika maadhimisho
hayo kwa waumini wa kanisa Katoliki (hawapo pichani) Parokia ya Mbangamao Jimbo
la Mbinga mkoani Ruvuma. (Picha zote na Julius Konala)
ASKOFU mkuu Damian Dallu, wa Jimbo kuu katoliki la
Songea mkoani Ruvuma ameipongeza Parokia ya Mbangamao iliyopo katika Jimbo la
Mbinga mkoani humo, kwa mchango wake mkubwa wa kusukuma maendeleo hususani
katika sekta ya elimu kwa kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka
1964 chini ya Paroko wake wa kwanza mzalendo Hayati Askofu Maurus Komba.
Askofu Dallu ametoa pongezi hizo wakati akiwahubiria mamia ya
waumini wa kanisa hilo kwenye maadhimisho ya Ibada ya misa takatifu ya shukrani,
Jubilei ya miaka 50 ya parokia hiyo iliyofanyika nje ya viwanja vya kanisa hilo
na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo maaskofu, mapadre, matawa, waumini
pamoja na viongozi wa serikali.
Alisema Parokia hiyo kupitia Shirika la Wavisenti imefanikiwa
kupanua wigo mkubwa wa kutoa huduma kwa jamii, ikiwemo kuongeza idadi ya shule
za msingi hadi kufikia 15, shule za sekondari tatu na ujenzi wa shule za
chekechea kwa kila kigango.
Vilevile ameeleza kuwa wameweza kutoa huduma ya maji safi na
salama kwa wakazi wa eneo hilo ikiwemo pamoja na parokia hiyo kuzaa parokia
mpya ya Mpepai iliyopo wilayani humo na kufanya ukarabati wa zahanati, shule za
msingi na ujenzi wa sekondari.
|
0 comments:
Post a Comment