Sunday, 3 August 2014

Pichani ni fukwe katika ziwa Nyasa eneo la Lundo Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.Hizi ni miongoni mwa fukwe  bora zenye vivutio adimu vya utalii,hata hivyo fukwe katika ziwa Nyasa bado hazijaendelezwa, zinahitaji wawekezaji ili kuinua sekta ya utalii wa ndani mwambao mwa ziwa Nyasa na ukanda wa kusini kwa ujumla

Na mathias pondamali .

UTAFITI ambao umefanyika katika ziwa Nyasa upande wa Tanzania na Malawi umebaini kuwa ziwa hilo linaoongoza ulimwenguni kwa kuwa na aina nyingi za samaki ukilinganisha na maziwa mengine duniani.
Kulingana na utafiti ambao ulifanywa na jumuiya ya nchi zilizo kusini mwa Afrika(SADC) kwa kushirikiana na  nchi ya Uingereza kwenye ziwa Nyasa kati ya mwaka 1991 hadi 1994 na mwaka 1996 hadi 2000,ulionesha kuwa ziwa hilo lina kiasi cha tani 165,000 za samaki na kati ya kiasi hicho tani 35,000 za samaki ni jamii ya samaki wa maji ya juu ambao wanaweza kuvuliwa bila kuathiri uvuvi kila mwaka.
Utafiti huo pia umebaini kuwa ziwa Nyasa ndiyo ziwe linaloongoza kwa kuwa na maji meupe kuliko maziwa yote ulimwenguni  huku likikamata nafasi ya tisa kwa ukubwa ulimwenguni ,na likiwa ni ziwa la tatu lenye kina kirefu zaidi ulimwenguni.Kutokana na utafiti huo ziwa Nyasa linatambulika kuwa ni sehemu ya urithi wa dunia.
Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania,Malawi na Msumbuji.Ziwa hilo lipo kwenye usawa wa meta 500 toka usawa wa bahari, kina cha ziwa hilo ni karibu meta 750,urefu wake ni karibu  kilometa 1000,upana mkubwa ni kilometa 80 na upana mdogo ni kilometa 15.

0 comments:

Post a Comment