Mgombea wa nafasi za Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema na mweka hazina, Jimbo la Muheza mkoani Tanga, Rashid Mhina amefariki ghafla wakati akihojiwa na wapigakura.
Mhina atazikwa leo jimboni humo, ambapo Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa anatarajiwa kuongoza mazishi hayo,
yatakayofanyika saa 8 mchana.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Grace Kiwelu aliliambia
gazeti hili jana kuwa tukio hilo lilitokea saa 7.30 mchana, wakati
wajumbe wa mkutano huo wakiwauliza maswali wagombea hao.
Kiwelu ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu
(Chadema), alisema katika uchaguzi huo Mhina alipata kura nane na
mshindani wake alipata kura 27 kwa nafasi ya mweka hazina, huku katika
nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Wazee alipata kura mbili kati ya
wagombea wanne hivyo kuwa wa mwisho.
“Tulianza na nafasi ya mweka hazina ambayo ilikuwa
na wagombea wawili, yeye (Mhina) na Claud Noel. Walianza kwa kuulizwa
maswali na kujibu, mgombea wa kwanza alikuwa Noel na Mhina alifuatia,”
alisema Kiwelu.
Aliongeza: “Alipoulizwa swali la kwanza, Mhina
alijibu, alipoulizwa swali la pili akapelekewa kinasa sauti ili ajibu,
ndipo alipodondoka chini na kupelekwa Hospitali Teule ya Muheza kwa
matibabu.”
Kiwelu alifafanua: “Niliwaeleza wanachama kwamba
tunaendelea na uchaguzi na hata kama Mhina yuko hospitali wampigie kura,
lakini baadaye uchaguzi ukiwa unaendelea, tuliletewa taarifa kwamba
amefariki dunia.”
Alisema kuwa baada ya taarifa hizo aliwasiliana na
Dk Slaa na kumweleza kilichotokea, ambapo aliwataka kuahirisha uchaguzi
wa jimbo hilo hadi utakapotangazwa tena.“Nimeshtushwa sana na tukio
hili kwani ni la kwanza,” alisema Kiwelu.
0 comments:
Post a Comment