Sunday 3 August 2014

Waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  Mansour Yusuph Himid akiwa  Makao Makuu ya Polisi Zanzibar jana, baada ya kukamatwa nyumbani kwake, Chukwani kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume na sheria.


Waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mansour Yusuph Himid amekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume na sheria imefahamika visiwani humo jana.
Mansour ambaye alivuliwa uanachama wa CCM na kupoteza nafasi ya mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Kiembesamaki, alikamatwa nyumbani kwake huko Chukwani na kufanyiwa upekuzi mkali na askari wa kikosi cha upelelezi wakiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Jeshi hilo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar Salum Msangi alisema Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za kiintelejensia kuwa waziri huyo wa zamani anamiliki silaha kinyume na sheria.
Msangi alisema mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Jeshi hilo lilianza kuifanyia kazi na jana ilikuwa siku rasmi ya kwenda kufanya upekuzi ndani ya nyumba yake na kufanikiwa kupata silaha aina ya Shortgun yenye namba za usajili 1904136413 aina ya Bore Browning pamoja na risasi 112.
Msangi alisema kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa silaha, hairuhusiwi kumiliki zaidi ya risasi 55 kwa silaha aina ya Shortgun na kueleza kuwa Jeshi hilo linaendelea kumhoji waziri huyo wa zamani.
Vilevile, Msangi aliongeza kuwa silaha nyingine aliyokamatwa nayo ni bastola yenye namba F76172W pamoja na risasi 295 jambo ambalo ni kinyume na sheria ya umiliki wa silaha za moto, ambapo mmiliki anatakiwa kuwa na risasi zisizozidi 25.

0 comments:

Post a Comment