Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea mjini mkoani Ruvuma, Josephat Ndulango. (Picha na Kassian Nyandindi) |
Songea.
CHAMA
cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mjini mkoani Ruvuma kimewanyoshea kidole
wanasiasa ambao wamekuwa wakiwatumia vijana kwa maslahi yao binafsi, kupitia mchakato
huu wa kutengeneza katiba mpya unaoendelea huko Bungeni badala yake kimewataka waachane
na ushabiki wa mambo ya kisiasa, na wawatumie vijana kwa maslahi ya taifa kwa
faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha
imeelezwa kuwa utengenezaji wa katiba mpya ni jukumu la Wabunge wa bunge maalum
la katiba, hivyo kwa wale waliokimbia mapambano bungeni ni kutowatendea haki
wananchi na ni dhambi ambayo itaendelea kuwatafuna kila siku maishani mwao,
badala yake warudi bungeni ili kuweza kumaliza misuguano inayoendelea kufukuta
na kuhatarisha ustawi wa maendeleo ya nchi yetu.
Katibu
wa CCM wilaya ya Songea mjini, Josephat Ndulango alisema hayo wakati alipokuwa
akizungumza na huu, huku akieleza kuwa vyama vya upinzani ndio vimekuwa
chagizo kwa kukataa kujenga maridhiano ya pamoja juu ya mchakato huo wa kuipata
katiba mpya.
“Wajibu
wao mkubwa ni kwenda bungeni na kutetea maslahi ya wananchi walio wengi wanapokimbia
mapambano sio suluhu, umoja wa wananchi wa katiba (UKAWA) ni muhimu warudi
bungeni kutengeneza katiba mpya”, alisema Ndulango.
Alisema
yeye ana amini kuwa endapo watarudi bungeni na kujenga ushirikiano wa pamoja
wataweza kutengeneza katiba ya Watanzania iliyo bora, ambayo itajali misingi ya
haki na ubinadamu kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ndulango
alisema utengenezaji wa katiba hii ni faida ya miaka 50 ijayo kwa taifa letu, hivyo
isipotengenezwa misingi imara huenda likawa ni tatizo au ombwe ambalo
litaendelea kuwagawa watanzania kwa namna moja au nyingine.
“Vurugu
na mifarakano ya hapa na pale kwa viongozi kulumbana kila kukicha haitakiwi,
kwa nini tusifikie mahali tukajenga misingi iliyo bora na yenye kuleta tija kwa
wananchi wetu?” , alihoji Ndulango.
Pia
alizungumzia kipengele cha haki za vijana kilichopo katika rasimu ya pili ya katiba
mpya, ambapo alieleza kuwa kimekuwa na mapungufu kwa kutoeleza bayana kijana ana
umuhimu gani, ni vyema wabunge wa bunge maalum la katiba wakakiweka sawa kwa
sababu jamii inatambua kuwa kijana ndio mhimili na msingi mkuu wa maendeleo ya
taifa hili.
Sambamba
na hilo Katibu huyo wa CCM vilevile amewataka viongozi wa chama hicho wilaya ya
Songea mkoani hapa, kuepukana na makundi yasiyo ya lazima badala yake kupitia
mikutano ya wananchi waeleze utekelezaji wa ilani ili kuweza kujenga misingi ya
kukiimarisha chama, na wananchi waweze kutambua nini kimewafanyia.
Ndulango
alisema Watendaji wa serikali katika maeneo mbalimbali wilayani humo baadhi yao
wamekuwa kikwazo katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, hivyo
wamesisitizwa kuacha kujiingiza kwenye mambo ya kisiasa badala yake wazingatie
majukumu yao ya kazi.
Hata
hivyo aliwaasa wananchi kupitia mchakato huu wa kuipata katiba mpya waache
mambo ya ushabiki wa kisiasa, hivyo waelekeze nguvu zao katika kusukuma mbele
gurudumu la maendeleo.
0 comments:
Post a Comment