Wednesday 13 August 2014

KATIKA hali isiyo ya kawaida, baadhi ya wakazi wa Tegeta, Dar es Salaam, wamekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumpitisha Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli awe mgombea wa chama hicho kwenye nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, kutokana na uchapakazi wake kwenye sekta ya ujenzi wa barabara nchini.

Wakazi hao walitoa ushauri huo jana wakati Dkt. Magufuli akiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Said Meck Sadick wakikagua barabara ya Mwenge-Tegeta, ambayo ujenzi wake umekamilika.

Katika ukaguzi huo, wakazi hao baada ya kumwona Dkt. Magufuli, walianza kumshangilia na kusema anafaa kuwa Rais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu 2015.

"Mheshimiwa wewe unafaa kuwa Rais, hongera sana kwa kutupunguzia foleni kwani una chapakazi...hakuna mwingine zaidi yako lakini barabara hii haina taa hivyo tunaomba utuwekee," walisema.

Akizungumza na wananchi hao, Dkt. Magufuli alisema maendeleo hayana itikadi ya chama chochote cha siasa wala dini  bali ni ya watu wote ambapo miradi yote ya ujenzi wa Barabara katika jiji hilo itagharimu sh. trilioni moja hadi kukamilika kwake.

Alisema kazi hiyo inafanywa na Rais Jakaya Kikwete kutoka na ushirikiano mzuri uliopo na mataifa mengine na barabara hiyo ataizindua mwenyewe kabla ya kuondoka madarakani ili asije Rais mwingine akasema yeye ndiye aliijenga.

"Baada ya miaka mitatu, jiji la Dar es Salaam halitakuwa na foleni tena kwani hivi sasa, barabara hii imekamilika kwa gharama ya sh. bilioni 89, katika bajeti ya mwaka huu, tumetenga sh. bilioni 2 ili kuiwekea taa  ila daraja lina uwezo wa kuhimili tani 180 lakini mnapaswa kutambua kuwa, hakuna vitamu bila uchungu," alisema Dkt. Magufuli.
Aliongeza kuwa, mbali ya barabara hiyo upanuzi wa Ujenzi wa Barabara ya Mwenge hadi Morocco, nao uko mbioni kuanza na ile ya kutoka Bagamoyo hadi bandarini ipo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuanza kazi ili kupunguza msongamano.

"Tupo katika hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa barabara za juu, kutakuwa na barabara za ghorofa tatu zinazopishana pale Ubungo na Tazara ambako ujenzi wake utaanza Oktoba mwaka huu, nyingine itakuwa Kamata, lengo ni kupunguza foleni," alisema.

Kwa upande wake, Bw. Sadick aliwaonya watu wanaohujumu miundombinu ya miradi ya Barabara baada ya kupewa taarifa kuwa sababu zinazosababisha Mkandarasi wa Barabara ya Mabasi yaendayo Kasi (DART), kushindwa kuikabidhi ni kutokana na watu kuiba taa.

Alisema hadi sasa, taarifa alizopewa taa saba na mabomba yake yameibwa ambapo mifuniko ya maji mchafu 12 na alama za barabara 25, nazo zimeibwa na watu wasio waaminifu.

"Ni marufuku kwa mtu yeyote kufanya biashara eneo la barabara ya mradi huo au kupumzika katika vituo vya mabasi haya...miradi hii inatumia fedha nyingi lakini watu wachache wanataka kuturudisha nyuma," alisema Bw. Sadick.

Naye Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada alisema Serikali ya nchi yake itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya barabara ili kupunguza tatizo la foleni nchini.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, alisema baadhi ya miradi ya barabara inakwamishwa na watu ambao tayari wamelipwa fidia lakini wanadai fidia waliyolipwa ni ndogo.

0 comments:

Post a Comment