Monday 11 August 2014

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira, amewapongeza wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kwa kuamua kurudi bungeni ili kuendelea na mijadala ya Rasimu.

Alisema wajumbe hao hawapaswi kubezwa bali wanastahili pongezi kwa kutambua umuhimu wa kutengeneza Katiba kwa maslahi ya nchi na Watanzania kwa ujumla.

Bw. Wassira aliyasema hayo juzi wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari wakati akitembelea Mabanda ya Maonesho ya Wakulima na Wafugaji maarufu kama Nanenane, katika Viwanja vya Nzuguni, mkoani Dodoma.

"Kilichofanywa na baadhi ya wajumbe wanounda UKAWA si dhambi bali ni wazalendo halisi... sioni sababu ya wajumbe hawa kuonekana wasaliti kwani Katiba tunayoitengeneza si ya chama cha siasa bali ya Watanzania wote," alisema.

Akizungumzia kamati yake namba sita katika Bunge hilo, alisema kesho wataendelea kujadili sura ya nne ambapo hadi sasa, wamejadili sura tatu ikiwemo inayohusu sera za Taifa ambazo ndio msingi wa kutengeneza sera na sheria kwa ajili ya kusimamia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wananchi.

"Sura ya tatu, inazungumzia maadili na miiko ya viongozi, kama unavyojua, kumekuwepo na manung'uniko juu ya ubadhirifu, rushwa na kumomonyoka kwa maadili nchini...baadhi ya watu wanafikiri wakipewa kazi na Serikali, wanajipanga jinsi ya kuiba badala ya kujituma kazini ili aweze kuzalisha," alisema.

Aliongeza kuwa, wajumbe wa kamati yake wameweka vifungu katika rasimu ambavyo vitakuwa vinaielekeza Serikali jinsi ya kuchukua hatua na namna ya kuweka vyombo ambavyo vitasimamia maadili pamoja na miiko ya uongozi

0 comments:

Post a Comment