Polisi imetajwa kuwa kinara kwa
rushwa katika sekta zote za huduma za serikali nchini.Kwa mujibu wa
muhtasari wa utafiti uliofanywa na Shirika Lisilo la Kiserikali la
Twaweza, polisi inaongoza kwa asilimia 94 ikifuatiwa na sekta za kisiasa
(91), afya (82) na kodi kwa asilimia 80.
Muhtasari huo uliotolewa jana baada ya utafiti wa
simu uliofanyika Juni mwaka huu pekee, ulitaja sekta nyingine kuwa ni
ardhi asilimia 79, elimu (70), Serikali za Mitaa (68) na maji asilimia
56.
Matokeo ya utafiti huo uliojumuisha wananchi 1,425
wa Tanzania Bara ambao walipigiwa simu kati ya Juni 9 na 25, ulizidi
kubainisha kuwa nusu ya Watanzania wanaamini kuwa mashirika yasiyo ya
kiserikali nayo pia yanajihusisha na rushwa.
Muhtasari huo unaoitwa Je, juhudi za serikali
zimesaidia vita dhidi ya rushwa? Mtazamo wa watu kuhusu rushwa nchini
Tanzania unazidi kubainisha kuwa zaidi ya robo tatu ya wananchi
wanaamini rushwa imekithiri kuliko miaka 10 ya nyuma.
“Wananchi tisa kati ya 10 wanaona rushwa inayotolewa kwa polisi ni kitu cha kawaida sana,” ilisema sehemu ya muhtasari huo.
Utafiti huo ulibainisha kuwa wananchi walitoa rushwa walipokutana na polisi na kati ya watano, watatu waliombwa rushwa.
Muhtasari huo uliongeza kuwa ni wananchi wawili tu
kati ya watano walilipa rushwa hiyo na wananchi asilimia mbili walitoa
rushwa wenyewe bila hata kuombwa.
Aina nyingine ya rushwa iliyoshamiri ni ile
inayotolewa wakati wa kutafuta kazi na mtu mmoja kati ya watatu aliombwa
malipo yasiyo rasmi alipokuwa akitafuta kazi.
“Hata hivyo, mara nyingi wananchi wana misimamo
imara kwenye rushwa; huombwa mara nyingi, lakini hutoa mara chache tu,”
ilisema sehemu ya muhtasari huo na kuongeza;
“Mtu mmoja kati ya 10 ameripoti kuwahi kutoa rushwa kwa ajili ya kupata kazi.”
Akielezea muhtasari huo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Twaweza, Rakesh Rajan alisema ni jambo la kusikitisha kuona Watanzania
wanakumbana na rushwa katika maisha yao ya kila siku licha ya jitihada
mbalimbali za serikali na wadau za kuitokomeza.
0 comments:
Post a Comment