Katapila likibomoa moja ya nyumba nne zinazomilikiwa na Mchungaji Getrude Rwakatare katika eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam jana.
WIZARA
ya Ardhi, Nyumba na Makazi jana imebomoa nyumba nne zilizojengwa ndani
ya kiwanja namba 314 zilichopo eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam
zinazomilikiwa na Mchungaji Getrude Rwakatare kwa tuhuma kuwa alivamia
eneo hilo.
Kazi
hiyo ya ubomoaji, ilitekelezwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi na
iliendeshwa kwa pamoja na maofisa wa Ardhi kutoka wizarani na Manispaa
ya Kinondoni, waliodai wamepewa agizo hilo na Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Alphayo Kidata
Mhandisi
wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya alidai wamepewa agizo na Katibu
huyo, kuvunja nyumba ndani ya kiwanja hicho, baada ya kubainika kuwa
eneo hilo siyo mali ya Rwakatare, hivyo hastahili kujenga mahali hapo.
Mhandisi
Mkuya alidai pamoja kutokuwa mmiliki halali wa eneo hilo, nyumba hizo
pia zimejengwa bila utaratibu, ikiwemo kupata kibali cha ujenzi kutoka
katika manispaa hiyo, suala linaloashiria kuwa kulikuwa na kitu
kimejificha.
“Sisi
kama manispaa tumekuja kutekeleza agizo la kubomoa kutoka kwa Katibu
Mkuu, kinachoonyesha ni kuwa aliyejenga eneo hili alivamia eneo la mtu
mwingine huku akijua wazi ni kinyume cha utaratibu” alidai Mkuya.
Alidai
matatizo ya uvamizi wa viwanja, yamekuwa ni jambo la kawaida hasa
katika Manispaa ya Kinondoni na kwamba wanaendelea kuyashughulikia kwa
lengo la kuyapatia ufumbuzi wa haraka.
Awali,
kazi hiyo ya ubomoaji ilitanguliwa na ‘vuta nikuvute’ baina ya
mwanasheria aliyedai kuwa anamwakilisha Rwakatare, Emmanumuel Muganyizi
na Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya kuhusu suala la
kubomolewa kwa nyumba hizo, zinazodaiwa kujengwa ndani ya kipindi
kisichozidi miezi miwili na kupauliwa kwa vigae.
Huku
akiwa na nyaraka mbalimbali za kesi, alidai kesi bado ipo katika
Mahakama ya Kinondoni. Muganyizi alisema anashangazwa na uamuzi huo
uliochukuliwa kwa madai kuwa suala hilo, halijapatiwa ufumbuzi wa
kisheria na Mahakama.
“Ninaamini
hiki kinachoendelea hapa ni sawa na uvunjifu wa amani, kesi bado ipo
mahakamani inapaswa iachwe iishe ndiyo uamuzi ufanyike. Kwa hili
mnalofanya sasa siyo sawa kabisa,” alisema Muganyizi.
Mwanasheria
huyo wa Rwakatare, awali aliingia katika mzozo na waandishi, akidai
kushangazwa na kitendo chao cha kutaka kuandika habari hiyo.
Alidai
habari hiyo haina manufaa kwa jamii, kwa kuwa inahusu madai ya mtu na
mtu. Kwa upande wake, mtu anayedai kuwa mmiliki wa kiwanja hicho,
aliyekuwepo wakati kazi ya uboaji ikiendelea, Janeth Kiwia, alidai
kiwanja chake kilivamiwa na kuanza kujengwa mwishoni mwa mwaka jana
wakati akiwa safarini kwa watoto wake nje ya nchi.
Alidai
kabla ya kuvamia eneo hilo, kulikuwa na nyumba ya vyumba vinne,
aliyokuwa akiijenga taratibu, ambayo hata hivyo ilibomolewa na msingi
wake kutumika kujenga moja ya nyumba hizo.
“Tayari
kulikuwa na nyumba iliyokuwa imefikia usawa wa rinta, lakini cha
kushangaza walipovamia waliibomoa na kujenga ya kwao, namshukuru Mungu
kwa kuwa haki imetendeka baada ya kuhangaika huku na kule kutafuta haki
yangu,” alidai Janeth.
Alidai
kitendo hicho, kimemfanya kujenga imani na Serikali kuwa inatenda haki,
bila kujali kuwa aliyekuwa akiporwa na mnyonge, huku akiitaka
kuwasafisha baadhi ya watendaji waliopo ndani ya wizara hiyo,
wanaoshirikiana na watu wabaya kutaka kupora haki za watu.
“Nilikuwa
sitarajii kama ningefanikiwa tena kupata kiwanja changu, namshukuru
Mungu haki imetendeka bila hata mimi kutoa Shilingi moja, naomba tusife
moyo na Serikali yetu kwa kuwa inafanya kazi,” alisisitiza Janeth.
Mwanasheria
aliyekuwa akisimamia kesi ya Janeth, Howard Msechu kutoka Kampuni ya
uwakili ya Homac, alidai mteja wake ndiye mmiliki halali wa kiwanja
hicho.
0 comments:
Post a Comment