JESHI la Wananchi Tanzania (JWTZ)
limeendelea kung’ara kimataifa, ambapo jana jeshi hilo lilitamkwa kuwa
miongoni mwa majeshi ya nchi za Afrika, yatakayounda Jeshi la Kulinda
Amani Afrika.
Taarifa za ndani kutoka Mkutano wa
Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali zaidi ya 50 za Afrika na
Marekani, ambao umehudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete, zimeeleza kuwa
moja ya kazi za jeshi hilo, itakuwa kuwa tayari wakati wowote,
kukabiliana na tishio la kiusalama ndani ya Afrika.
Taarifa za Shirika la kimataifa la
habari la Reuters, zilizotolewa jana, zilieleza kuwa Serikali ya
Marekani katika mkutano huo uliomalizika juzi, imejipanga kutumia Dola
za Marekani milioni 110 kila mwaka kwa miaka mitatu mpaka mitano ijayo,
kusaidia jeshi hilo kufanya kazi kwa haraka katika maeneo yanayokabiliwa
na tishio la usalama na amani Afrika.
Hivi karibuni vikao vya JWTZ
vinavyolinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),
vilitajwa kuwa miongoni mwa vikosi bora 35 vya majeshi ya nchi
mbalimbali duniani, vinavyokubalika kwa kuwa na ufanisi wa hali ya juu,
uwezo mkubwa wa kupigana na vilivyofundishwa vizuri.
Mtandao wa Kimataifa wa Imgur Via
Distractify, ulieleza kuwa Tanzania ni nchi pekee ya Afrika, yenye jeshi
ambalo ni miongoni mwa majeshi bora 35 duniani.
Mwandishi, Micky Wren aliandika katika
mtandao huo kuwa, majeshi hayo, ikiwemo JWTZ yamefundishwa kwa kiwango
cha juu, yana silaha za kisasa na yameandaliwa vizuri kwa ajili ya
operesheni ngumu za kijeshi.
Pia, majeshi hayo yalitajwa kuwa yenye
uwezo wa kukabiliana na adui katika mazingira yoyote, kuanzia kumaliza
uhuni wa utekaji hadi kusambaratisha wahalifu wenye uwezo mkubwa.
Mwandishi huyo alitaja majeshi hayo
katika orodha ambayo haikupangwa kwa mtitiriko wa uwezo wa kijeshi,
ambapo mbali na JWTZ mengine ni Kikosi cha Seal cha Jeshi la Maji la
Marekani na Kikosi cha SAS cha Jeshi la Uingereza.
Kipo pia Kikosi cha Huntsmen Corps cha
Majeshi Maalumu ya Denmark, Majeshi Maalumu ya Ufaransa, Kikosi cha
MARSOC, Majeshi Maalumu ya Taiwan ambayo yanatumia kinga za usoni
zisizoweza kuingiliwa na risasi na Kikosi cha Irish Army Rangers cha
Jamhuri ya Ireland.
Vingine ni Gendarmerie cha Serbia,
Kikosi Maalumu cha Kukabiliana na Ugaidi cha JTF2 cha Canada, Majeshi
Maalumu ya Uholanzi, Kikosi cha SBS, Majeshi Maalumu ya Jamhuri ya Korea
na Majeshi Maalumu ya Ufaransa.
Pia, yapo Majeshi Maalumu ya Ubelgiji,
Kikosi cha MJK cha Norway, Canadian Joint Response Unit cha Canada,
Majeshi Maalumu ya Norway, Kikosi cha French Commando Marine, Majeshi
Maalumu ya New Zealand, Kikosi cha Norwegian Armed Forces Special
Command na Kikosi cha Polish Grom cha Poland.
Vingine ni Kikosi cha US Army Special
Forces Sniper with Remington Modular Sniper Rifle, Majeshi Maalumu ya
Marekani, Majeshi Maalum ya Indonesia, Majeshi Maalum ya Romania na
Kikosi cha SASR cha Australia.
Kikosi cha KSK cha Ujerumani, Majeshi
Maalumu ya Ujerumani, Majeshi Maalumu ya Israel – Shayetet 13, Majeshi
Maalumu ya Urusi – Spetsnaz, Majeshi Maalum ya Austria – Jagdkommando,
Majeshi Maalumu ya Iraq, Majeshi Maalumu ya Ujerumani ya SEK-M na
Majeshi Maalumu ya Peru.
Maofisa wa Serikali ya Marekani,
wamekaririwa na Reuters wakieleza kwamba mbali na Tanzania, majeshi
mengine yatakayounda jeshi hilo yanatoka nchi za Senegal, Ghana,
Ethiopia, Rwanda na Uganda.
“Tumeshuhudia kwa muda mrefu sasa
majeshi ya nchi za Afrika, yakifanya kazi kwa weledi katika maeneo yenye
migogoro,” ilisema Reuters ikimkariri ofisa mmoja wa Serikali ya
Marekani.
Ofisa huyo alisema pamoja na mafanikio
ya majeshi hayo ya Afrika, bado kumeendelea kujitokeza changamoto ya
kusaidia vikosi vya majeshi hayo, kuingilia kati sehemu zenye migogoro
kwa haraka zaidi, pamoja na namna ya kujilinda na kujikimu wakiwa katika
majukumu hayo ya kimataifa.
Kutokana na changamoto hizo, fedha hizo
zinazofikia Dola milioni 550 baada ya miaka hiyo mitano, zinatarajiwa
kuanza kutolewa mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa Marekani unaoanza Oktoba
mwaka huu, na zitapelekwa moja kwa moja, kusaidia utendaji wa haraka wa
jeshi hilo, katika maeneo yanayokabiliwa na tishio la kuibuka kwa
migogoro.
0 comments:
Post a Comment