Jeshi la Polisi linamshikilia Inspekta wake, Celestine Makene (40) kwa madai ya kumpiga hadi kumsababishia kifo mtoto wa kaka yake, Alerd Makene (16).
Makene anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 24, mwaka
huu katika makazi ya polisi, Mtoni Kijichi, Dar es Salaam na
anashikiliwa katika Kituo cha Chang’ombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya wa
Kihenya alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema marehemu Alerd
alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari
Mbagala Kuu.
Hata hivyo, alisema uchunguzi wa kifo chake
unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa endapo
itathibitika kuwa alitenda kosa hilo.
“Tunamshikilia mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye pia
ni askari polisi katika Chuo cha Polisi Kurasini, tutahakikisha kuwa
haki inatendeka bila kujali nafasi aliyonayo mtuhumiwa,” alisema kamanda
huyo.
Imedaiwa kuwa Makene alimwadhibu baada ya kupokea
malalamiko kutoka kwa mzazi wa jirani akimlalamikia kwamba Alerd
alimpiga mwanaye hivyo kumtaka amkanye juu ya tabia hiyo.
Akizungumzia tukio hilo, jirani ambaye hakutaka
jina lake kutajwa gazetini, alisema watoto hao walikuwa wakicheza mpira
lakini kwa bahati mbaya Alerd alimpiga rafiki yake huyo usoni kwa mpira
na baada ya kupigwa kwa mpira, alikwenda kwao kumshtaki.
“Usiku huo baba yake alimfungia chumbani na
kumpiga kwa fimbo, ngumi na mateke kiasi kilichomfanya mtoto huyo kupiga
kelele sana,” alisema na kuongeza kwamba majirani walijaribu kwenda
kumwamulia lakini hakusikiliza.
Alisema siku iliyofuata mtuhumiwa alisafiri kikazi
Nairobi lakini akadai kuwa kabla ya kuondoka, aliamuru mtoto huyo
asifunguliwe mlango.
Alidai kuwa baada ya mtoto huyo kulalamika sana,
mama yake mdogo alimfungulia mlango na kumkuta akiwa amevimba uso na
akivuja damu nyingi.
Alisema waliamua kumpeleka Hospitali ya Temeke kwa matibabu na alifariki dunia usiku wa Ijumaa Agosti Mosi.
“Baba yake alirudi haraka kutoka Nairobi
alipopigiwa simu kuwa Alerd ana hali mbaya na alifahamishwa baada ya
muda mfupi kuwa amefariki,” alisema.
0 comments:
Post a Comment