Rais
wa TFF, Jamal Emil Malinzi aliaminiwa na Watanzania wengi kuongoza
soka, lakini kuna changamoto nyingi zinazomkabili kiutendaji
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) jana
limetangaza kuongeza muda wa usajili kwa wiki mbili ili kuzipa klabu nafasi ya
kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
Katika taarifa yake, TFF ilisema hatua ya kwanza
ya usajili inakamilika Agosti 17 mwaka huu badala ya Agosti 3 ya awali.
Kutokana na marekebisho hayo, kipindi cha uhamisho
kinakamilika Agosti 17 mwaka huu wakati pingamizi itakuwa kati ya Agosti 19
hadi 26 mwaka huu.
Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
itathibitisha usajili kati ya Septemba 1 na 2 mwaka huu.
Uhamisho wa kimataifa, usajili wa wachezaji huru,
na utatuzi wa dosari za usajili unatakiwa uwe umekamilika kufikia Septemba 7
mwaka huu. Uthibitisho wa hatua ya mwisho ya usajili utafanywa Septemba 15
mwaka huu.
Kwa upande wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa
2014/2015 itaanza Septemba 20 mwaka huu, na ratiba itatolewa mwezi mmoja kabla
ya kuanza ligi hiyo.
Mwenyekiti
wa kamati ya usajili wa Simba sc, Zacharia Hans Poppe ameongezewe wiki
mbili na TFF kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
Utaratibu huu wa kuongeza-ongeza muda umezoeleka
nchini Tanzania na kufikia hatua kuonekana kama ni ‘kasheria’ fulani. Mazoea
hujenga tabia, ‘walishasemaga’ wazee wa zamani. Moja ya kanuni ya maisha ni
kuzingatia muda na kufuata mipaka uliyojiwekea.
Kama umepanga kufanya kazi kwa saa nne, basi
ikifika muda huo inabidi uache, labda kama kumetokea sababu ya msingi, hapo
unaweza kuongeza muda zaidi.
Barani ulaya, sheria zinaheshimika sana ikiwemo
hii ya dirisha la usajili. Siku zote sipendi kuifananisha Tanzania na Ulaya,
hatuwezi kuwa kama wao, lakini kuna vitu vyepesi vya kuwaiga kama hili la
kwenda na muda.
TFF wanaongeza muda wa usajili na ukisoma sababu
yao ni kuzipa klabu nafasi ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa. Kwani klabu
haziwezi kukamilisha taratibu hizo ndani ya muda uliopangwa? lazima ziongezewe
muda?
Haya
sasa Seif Ahmed `Magari` (mwenyekiti wa kamati ya mashindano na mjumbe
wa kamati ya usajili Yanga sc) fanyeni yenu, TFF wamewapa muda wa wiki
mbili zaidi wa kusaka wachezaji
Kwa mtazamo wa haraka haraka, kuongeza muda
imekuwa mazoea. Sidhani kama ni sheria, lakini TFF wanaongozwa zaidi na busara
kufanya maamuzi na sio sheria.
Unaweka siku ya mwisho ya usajili (Deadline) kuwa
ni Julai 15, muda unafika unatokea hadharani ukisema: “Nimeongeza muda kwa wiki
mbili ili klabu zikamilishe taratibu”. Kwanini wasikamilishe ndani ya muda uliopangwa
na kama watashindwa kwanini wasichukuliwe hatua au waachwe na timu zao `mbofu
mbofu`.
Ni jambo rahisi tu kubaki katika misingi ya kanuni
ili tuepukane na mazoea. Naamini wapo viongozi wa klabu huwa hawahangaikii
usajili ndani ya muda uliopangwa kwasababu wana uhakika kuwa TFF itaongeza
muda.
Kiongozi hasajili, akiulizwa kwanini? Utasikia muda bado upo, tunafanya mambo
yetu polepole. Ukiangalia muda unaosema upo, unagundua unakaribia kwenye siku
ya mwisho (Deadline). Ni rahisi kujua kuwa kuna baadhi ya watu wanakuwa wanajua
kabisa kwamba TFF wataongeza muda.
Huku ni kuwazoesha watu kutofuata kanuni na
sheria. Kwanini watu wazembee kwa madai ya kuongezewa muda.
Mabingwa Azam fc nao hawajakamilisha usajili?
Wenzetu hawana taratibu za hivyo. Siku ya mwisho
ya usajili, makocha wanahaha kama hawajakamilisha. Unakumbuka usajili wa Mesut
Ozil kujiunga na Asernal kitokea Real Madrid?. Aserne Wenger alijua kabisa inakula kwake, muda umekwisha na hajafanya
mambo.
Unadhani Wenger aliwahi kuwaza kuwa muda wa
usajili utaongezwa?, lakini kwa Bongo ndio kwanza watu wanalala na kuendelea na
maisha mengine, huku `Deadline` ikikaribia.
Ifike wakati TFF ibaki katika misingi ya kanuni
ili kuondoa usemi wa `Hii ni Afrika` yaani `This is Africa`. Tusipende kujipa
mazoea nje ya kanuni.
Kila siku tunajadili kuendeleza soka, tunaangalia
upande mmoja wa tu yaani mpira wa uwanjani, hata suala la kuzingatia kanuni na
sheria ni sehemu ya mchezo.
Leo hii huwezi ukawa unaongeza muda bila sababu ya
msingi, mara ratiba inawekewa viraka, mara inasogezwa mbele zaidi bila kuwa na
sababu ya msingi.
Kwa mfano mwaka huu ratiba imesogezwa kutoka
Agosti 24 mpaka septemba 20 mwaka huu. Sababu kubwa ni kuipisha Yanga
itakayoenda kushiriki kombe la Kagame nchini Rwanda kuanzia Agosti 8 mwaka huu.
Kama Yanga watafika fainali, maana yake watamaliza
mashindano hayo Agosti 24 ambayo ndio siku ya fainali kwa mujibu wa ratiba
iliyotolewa na CECAFA siku ya jana.
Lakini kama Yanga watatolewa hatua ya makundi, maana
yake watarudi nchini kati ya Agosti 17 au 18 kwasababu mechi ya mwisho ya
makundi itakuwa Agosti 16 dhidi ya Coffee ya Ethipopia.
Kama watapambana na kufika fainali, maana yake
Kagame ingemalizika siku ambayo ligi inaanza kwa mujibu wa kalenda ya awali ya
TFF.
Lakini kwasababau hiyo ya kombe la Kagame, TFF
wakasogeza ligi mpaka septemba 20. Ukiangalia hapa, ni siku 26 zaidi baada ya
kagame kumalizika. Hivi sababu ni Kagame au ndo mpaka haya mambo ya usajili?
Wakati taarifa ya kusogeza mbele ligi kuu
inatolewa na TFF, ilielezwa kuna sababu mbalimbali za kufikia maamuzi hayo,
lakini kubwa ni kuisubiri Yanga.
Sababu mbalimbali hazikuweka wazi kwa kumbukumbu
zangu, lakini sasa nimegundua kuwa ni pamoja na klabu kutokamilisha usajili.
Hii ni tabia isiyofaa kuendelea. Rais wa TFF, Bwana
Jamal Emil Malinzi, umeaminiwa na Watanzania wengi, japokuwa kumekuwepo na
dosari za hapa na pale kiutendaji, futa mazoea ya kutoka kwenye kanuni.
Sioni sababu ya kuongeza muda wa usajili, lazima
tufuate kanuni. Najua ligi yetu ni fupi sana na ndio maana inapigwa pigwa
kalenda, lakini kuna njia nyingine ya kufanya ikiwa ni pamoja na kurudisha
mashindano kama Taifa Cup na mengineyo.
Nadhani kuna watu wa klabu wapo TFF, kwahiyo
wanafanya maamuzi kwa maslahi binafsi na kuja hadharani kama TFF.
Watu hawa wanakuja na suala la kuongeza muda eti
klabu hazijakamilisha taratibu. Mbona kuna timu zimemaliza kusajili?
Mazoea yana taabu. Ukishazoea kufanya kitu kinyume
na taratibu, utaona kanuni na sheria ni adau yako.
Ramadhani Karim!
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment