Friday, 5 September 2014

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC) kuhakikisha kuwa nyumba za gharama nafuu zinazojengwa kwa ajili ya makazi zinakidhi mahitaji ya familia.
Balozi Seif Idd alitoa mwito huo mjini Singida mara baada ya kutembelea shughuli za ujenzi wa nyumba 20 katika eneo la Unyakumi, Manispaa ya Singida, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa nyumba 15,000 zinazojengwa na shirika hilo kote nchini kwa ajili ya makazi.
Alisema ingawa baadhi ya mashirika yamekuwa na nia njema ya kusaidia wananchi kumiliki nyumba kwa bei nafuu badala ya kuendelea kupanga, baadhi ya nyumba zinazojengwa ni ndogo kiasi cha kutokidhi mahitaji ya wanafamilia wanaonunua, wengi wao wakiwa wastaafu.
Kutokana na hali hiyo, Balozi Idd alisema kuwa ipo haja kwa Shirika hilo la Nyumba nchini kuhakikisha kuwa nyumba 15,000 zinazoendelea kujengwa kote nchini zinakuwa na ubora na viwango vinavyokidhi mahitaji ya familia.
Kaimu Meneja wa NHC Mkoa wa Singida, Peter Luheja alisema kuwa zaidi ya Sh milioni 900 zitatumika kugharimia ujenzi wa nyumba hizo 20 katika eneo la Unyakumi, Manispaa ya Singida.
Luheja alisema kuwa mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika Manispaa ya Singida unatarajiwa kukamilika na nyumba kuanza kuuzwa kwa wananchi ifikapo Oktoba mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment