Friday 5 September 2014

Picha Na 2Mwenyekiti wa Jopo la Majaji kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji Prof. Samwel Wangwe (kushoto) akisalimiana na Afisa Mahusiano wa Mgodi wa North Mara Bw. Zakayo Kalebo (kulia) mara baada ya jopo hilo kuwasili kwenye mgodi huo.
Picha Na 3Meneja Mahusiano wa Mgodi wa North Mara Bi Fatuma Mssumi (mbele) akielezea shughuli za mgodi wa North Mara mbele ya jopo la majaji waliotembelea mgodi huo ili kuendelea na zoezi lake la kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji.
Picha Na 5Afisa Uhusiano wa Kijiji cha Matongo Bw. Magesa Wanjara akionesha jinsi ya kutumia bomba la kisima cha maji kilichofadhiliwa na mgodi wa North Mara mbele ya timu ya majaji, sekretarieti na wajumbe wengine.
Picha Na 7Mwenyekiti wa Umoja wa Kikundi cha Vijana cha Nyakegema Bw. Zacharia Mwita ( wa pili kutoka kulia) akitoa maelezo mbele ya timu ya majaji na wajumbe wengine kuhusu mchango wa mgodi wa North Mara kwa kikundi hicho kupitia mradi wake wa mboga za majani. Kikundi hicho kina jumla ya vijana 578 kutoka katika vijiji saba vinavyouzunguka mgodi huo.
Picha Na 9Mwenyekiti wa Jopo la Majaji kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji Prof. Samwel Wangwe (kushoto) akisalimiana na Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ingwe Bw. Alfred Joseph mara timu hiyo ilipofanya ziara kwenye shule hiyo iliyofadhiliwa na mgodi wa North Mara.
……………………………………………
Imeelezwa kuwa mgodi wa North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara umechangia jumla ya shilingi bilioni 7.5 katika kipindi cha mwaka 2013 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo   katika vijiji saba vinavyouzunguka mgodi huo.
Akizungumza mbele ya timu ya majaji kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji chini ya mwenyekiti wake Prof. Samwel Wangwe Meneja Mahusiano wa Mgodi huyo Bi Fatuma Mssumi alitaja vijiji hivyo kuwa ni pamoja na Nyangoto, Nyamwaga, Nyakunguru, Kerende, Kewanja, Genkuru na Matongo.
Bi Mssumi alisema kuwa kupitia sekta ya elimu, mgodi ulichangia madawati 2700 yenye thamani ya shilingi milioni 251.9 kwa ajili ya shule mbalimbali za msingi na sekondari na kuongeza kuwa mgodi ulijenga shule ya sekondari ya Ingwe kwa shilingi bilioni 1.1 miradi ambayo imekamilika.
Alisema kuwa mgodi ulifanya ukarabati pamoja na ujenzi wa shule ya sekondari ya Kemambo kwa gharama ya shilingi milioni 905.5, na shule ya msingi ya Bong’eng’e kwa gharama ya shiligi milioni 827.
Aliongeza kuwa mgodi huo katika awamu yake ya kwanza ulichangia shilingi milioni 605. 8 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Nyamwaga mradi ambao bado unaendelea.
“ Pia   mgodi uligharamia shilingi milioni 12.7 kwa ajili ya wanafunzi waliofanya vizuri kusoma katika shule na vyuo mbalimbali”, alisema Bi Mssumi
Aliongeza kuwa nia ya kuwekeza katika elimu katika wilaya ya Tarime ni kuhakikisha wanajenga msingi utakaopelekea kupatikana wataalamu kwa ajili ya kufanya kazi katika mgodi huo.
Akielezea mchango wa mgodi huo katika sekta ya afya Bi Mssumi alitaja miradi mingine kuwa ni pamoja na ukarabati na ujenzi wa zahanati ya Genkuru uliogharimu shilingi milioni 61.2, upimaji wa macho kwa wanakijiji 3,000 kwa shilingi milioni 19 pamoja na upimaji wa virusi vya Ukimwi kwa wanakijiji 1067 uliogharimu shilingi milioni tano.
Aliendelea kusema kuwa mgodi huo ulitoa msaada kwaajili ya upasuaji kwa wanakijiji 11 ambapo jumla ya shilingi milioni 12.2 zilitumika
Akielezea sekta ya maji Bi. Mssumi alisema kuwa mgodi ulichimba visima katika vijiji sita kwa thamani ya shilingi milioni 888.3 pamoja na usambazaji wa maji katika vijiji vya Nyangoto, Kewanja, Matongo na Kerende uliogharimu shilingi bilioni 1.2
Alisema kuwa mgodi pia ulifanya ukarabati katika kituo cha afya cha Nyangoto kwa gharama ya shilingi milioni 481.7 pamoja na usafi katika vijiji vya Nyangoto, Kerende, Kewanja na Nyamwaga uliogharimu shilingi milioni 544.4
Alisisitiza kuwa ili kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wananufaika na sekta ya madini kupitia kujiajiri mgodi huo ulichangia shilingi milioni 91.4 kwa kikundi cha wachimbaji wadogo Tarime kwa ajili ya ununuzi wa mashine kwa ajili ya kusaga kokoto.
Bi Mssumi aliongeza kuwa hatua iliyofikiwa sasa ni mkandarasi kufanya kazi ya kutoa umeme kutoka mgodi wa North Mara hadi mashine ilipo ili ianze kazi mara moja.
Alisema kuwa mgodi pia ulifadhili   miradi mbalimbali kwa gharama ya shilingi milioni 252.5 pamoja na vikundi vya kijamii/kidini kwa gharama ya shilingi bilioni 1.8
Akizungumzia mchango wa mgodi huo katika sekta ya miundombinu Bi Mssumi alisema kuwa mgodi huo ulikarabati barabara yenye urefu wa kilomita 47.9 kwa gharama ya shilingi milioni 469 pamoja na uunganishaji wa umeme kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) katika vijiji vya Kerende na Matongo kwa gharama ya shilingi milioni 472
Alitaja miradi mingine kuwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi uliogharimu shilingi milioni 555.5 na ujenzi wa mahakama ya mwanzo Nyamongo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa mahakama hiyo kwa shilingi milioni 182.9 mradi ambao haujakamilika bado.
Akizungumzia changamoto katika   utekelezaji wa miradi hiyo, Bi. Mssumi alisema kuwa kumekuwepo na tatizo la wanavijiji kuhujumu miundombinu ya maji iliyowekwa hali inayopelekea mgodi huo kuingia gharama kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu hiyo.
“Wapo wanakijiji wasio waaminifu ambao huharibu miundombinu ya maji kwa makusudi ili kufanya biashara ya maji jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya vijiji hivyo” Alisisitiza Bi. Mssumi

0 comments:

Post a Comment