Friday, 19 September 2014

 

pix 1Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo (mwenye shati la batiki), akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito wa Thailand, walipotembelea Banda la Tanzania katika Maonesho ya 54 ya Vito na Usonara ya Bangkok, yaliyofanyika Septemba 9 hadi 13 mwaka huu.
pix 2 
 
Makamu wa kwanza wa Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito na Usonara wa Thailand, Bw. Sutipong Dumrongsakul, akimkabidhi zawadi maalumu Mkuu wa Ujumbe kutoka Tanzania ulioshiriki maonesho ya vito ya Bangkok, Archard Kalugendo, mara baada ya kikao kati ya Ujumbe huo na Viongozi wa Taasisi hiyo ya Wafanyabiashara wa Thailand.
pix 3 
Wateja mbalimbali wakihudumiwa katika Banda la Tanzania kwenye maonesho ya vito na usonara ya Bangkok yaliyofanyika hivi karibuni nchini Thailand.Baadhi ya Watanzania walioshiriki maonesho ya vito na usonara nchini Thailand, wakimsikiliza mmoja wa wateja aliyetembelea Banda la Tanzania.
pix 5 
Ujumbe wa Tanzania (Kulia) wakiwa katika kikao na Uongozi wa juu wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito na Usonara wa Thailand, ambao ndiyo waandaaji wa maonesho ya vito na usonara ya Bangkok.
pix 6 
Baadhi ya Watanzania walioshiriki maonesho ya vito na usonara ya Bangkok, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungwa rasmi kwa maonesho hayo.
pix 7Watanzania walioshiriki maonesho ya vito na usonara ya Bangkok walitumia fursa ya maonesho hayo kutangaza pia utamaduni na vivutio mbalimbali vya utalii vipatikanavyo nchini Tanzania. Pichani ni Eva Mowo (kushoto) Afisa kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Lightness Makundi, Afisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini wakiwa wamevalia mavazi ya kimasai.
pix 8 
Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika maonesho ya vito na usonara ya Bangkok pia walitumia fursa ya maonesho hayo kutangaza maonesho ya vito ya Arusha yanayotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu jijiji Arusha. Pichani ni Eva Mowo, Afisa kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Lightness Makundi, Afisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wakiwa wamepozi katika bango lenye ujumbe wa kutangaza maonesho ya Arusha. Maafisa hao walivalia mavazi ya asili (vitenge) na mikufu yenye vito vya Tanzanite kutangaza utamaduni wa Kitanzania na madini hayo maarufu ya vito yapatikanayo Tanzania pekee.  
pix 9 
Makamu wa Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito – Thailand, ambao ndiyo waandaaji wa Maonesho ya Vito ya Bangkok, Tony Brooke akizungumza na baadhi ya Watanzania walioshiriki katika Maonesho hayo nchini Thailand alipotembelea Banda la Tanzania. Sambamba naye (mwenye shati la kitenge) ni Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania katika maonesho hayo, Archard Kalugendo.
 
Tanzania, Thailand kushirikiana katika madini vito

Wafanyabiashara wa madini ya vito na usonara wa Thailand wameonyesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika sekta hiyo kwa lengo la kukuza uhusiano na kuzinufaisha pande zote mbili.
Hayo yalibainika hivi karibuni katika kikao kilichokutanisha Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Maonesho ya Vito na Usonara yaliyofanyika Bangkok nchini Thailand na Uongozi wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa madini hayo kutoka nchini humo.
Akiwasilisha  maoni na mapendekezo kutoka upande wa Tanzania katika kikao hicho, Kiongozi wa Ujumbe kutoka Tanzania, Archard Kalugendo ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), alisema Tanzania inapenda kushirikiana na Wa-Thailand katika sekta hiyo ili pamoja na mambo mengine kuiga na kujifunza kutoka kwao.
“Ninyi wenzetu mmeendelea sana katika sekta hii ya madini ya vito na usonara. Tunapenda kujifunza na kuiga kutoka kwenu ili nasi tufike hapo mlipofikia na hata zaidi ya hapo,” alisema Kalugendo.
Aliongeza kwamba, lengo la Serikali ya Tanzania ni kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha inawawezesha wananchi wake hususan wanaojishughulisha na biashara ya madini ya vito na usonara ili wanufaike ipasavyo kupitia kazi hiyo na pia kulinufaisha Taifa kwa ujumla kwa kukuza uchumi wa nchi.
Alisema, Serikali inayo nia na imejipanga kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito na usonara katika Bara la Afrika na kwamba inatumia njia mbalimbali kufanikisha hilo ikiwemo kuendelea kuboresha Maonesho ya Vito na Usonara ya Arusha (Arusha Gem Fair – AGF) yanayofanyika kila mwaka.
Kalugendo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Wafanyabiashara wa Thailand katika Maonesho ya Vito ya Arusha yanayotarajiwa kufanyika mapema mwezi Novemba mwaka huu jijini Arusha.
“Tanzania inayo mazingira mazuri sana ya uwekezaji na ninawahakikishia kuwa ushiriki wenu katika maonesho hayo utakuwa wenye tija kwenu na kwetu pia,” alisema.
Aidha, Kalugendo alitoa maombi ya Tanzania kupatiwa nafasi kubwa zaidi katika Maonesho ya Vito na Usonara ya Thailand ili washiriki wengi zaidi wakiwemo wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hayo waweze kushiriki na kujipatia uzoefu utakaowasaidia kuboresha utendaji wao na hivyo kumudu ushindani katika soko na viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Maonesho ya Vito na Usonara ya Arusha, Peter Pereira alisisitiza umuhimu wa Thailand kushiriki katika maonesho ya Arusha na kuwahakikishia kuwa mazingira mazuri yameandaliwa kwa ushiriki wenye tija ikiwemo kuondoa gharama za kodi ya thamani katika bidhaa (VAT) kwa kipindi chote cha maonesho.
Akijibu hoja na mapendekezo kutoka upande wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito – Thailand, ambao ndiyo waandaaji wa Maonesho ya Vito ya Bangkok, Tony Brooke alisema Thailand inapenda kushirikiana kwa ukaribu zaidi na Tanzania katika sekta hiyo.
Alisema Wafanyabiashara wa Thailand watashiriki katika maonesho ya vito ya Arusha na kuahidi kuboresha ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya vito ya Bangkok.
Brooke alitoa changamoto kwa Tanzania kujiandaa vema zaidi katika ushiriki wa maonesho kama hayo kwa kuhakikisha inapeleka madini na bidhaa kwa wingi kulingana na uhitaji wa wateja.
“Wateja wengi wanatembelea banda la Tanzania kuliko madini na bidhaa zilizopo. Ongezeni wingi wa bidhaa maana uhitaji ni mkubwa,” alisisitiza Brooke.
Alikubaliana na wazo la kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha madini ya vito na usonara katika bara la Afrika na kusisitiza kufanya kazi kwa bidii, weledi na kujituma kwa hali juu ili kuhakikisha lengo hilo linatimia.
“Hatua mnayoona tumefikia katika sekta hii ya madini ya vito na usonara imekuja kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na kujituma, hivyo nanyi ili mfanikiwe mnapaswa kufanya hivyo,” alisema.
Nchi ya Thailand ina uzoefu wa miaka 40 katika biashara ya madini ya vito na usonara na imekuwa ikiandaa maonesho makubwa kila mwaka katika kipindi hicho chote ili kuuza bidhaa zitokanazo na madini ya vito na kujitangaza zaidi kimataifa.
Maonyesho ya Vito na Usonara ya Bangkok kwa mwaka huu yalifanyika kuanzia Septemba 9 hadi 13 na kushirikisha mataifa mbalimbali duniani.

0 comments:

Post a Comment