Mkurugenzi
wa Habari, Elimu kwa Umma na Itifaki wa Bunge Maalum la Katiba, Bw.
Jossey Mwakasyuka (kushoto) akisisitiza jambo wakati wa semina
iliyoandaliwa kwa ajili ya waandishi wa habari kuhusu kuimarisha
Uandishi wa Habari za shughuli za Bunge iliyofanyika tarehe 6 Septemba,
2014 katika Ukumbi wa African Dreams mjini Dodoma. Kulia ni Mshauri wa
mambo ya Kiufundi toka Shirika la Kimataifa la UNDP, Bi. Anna
Kochannesyan.
Kanuni za Bunge Maalum hususani
Kanuni ya 77 inawataka waandishi wa habari kuandika habari za Bunge
Maalum kwa weledi mkubwa na kuzingatia maadili ya uandishi wa habari ili
kujiepusha na uandishi wenye utashi na ushabiki wa kisiasa, msukumo
binafsi, chuki ama uchochezi na wakati mwingine uongo wa makusudi.
Aidha, katika Kanuni hiyo hiyo ya 77(3) inatamka bayana ya kuwa “Katibu
anaweza wakati wowote kuondoa ruhusa aliyotoa kwa mwakilishi wa Chombo
chochote cha habari iwapo chombo hicho kitatoa taarifa yoyote kuhusu
shughuli za Bunge Maalum ambayo kwa maoni ya Bunge Maalum inapotosha
ukweli au vinginevyo inakiuka Kanuni, taratibu au haki za Bunge Maalum”.
Vyombo vya habari vina haki ya
kupata habari ili viweze kuhabarisha umma juu ya mambo mbalimbali
yanayoendelea nchini has katika Bunge Maalum la Katiba, lakini katika
kufanya hivyo waandishi wa habari wanapaswa kutenganisha kati ya siasa
na uandishi wa habari, hivyo wanapaswa kubainisha na kuainisha dhana ya
uandishi wa habari za kibunge wenye tija kwa taifa ambayo ni weledi
katika uandishi wa habari, uelewa kuhusu matarajio ya wananchi pamoja na
uelewa juu ya dhima na dhamira ya Bunge katika taifa.
Uandishi wa habari ni vema
usitumiwe kama njia ya kufikia malengo ya kisiasa ama mtu binafsi,
makundi au chama na kitendo cha mwanasiasa kuvaa koti la uandishi wakati
ni mwanasiasa kunajenga chuki, kunaharibu heshima ya uandishi wa habari
na maisha ya waandishi.
Endapo siasa zitaingizwa katika
uandishi wa habari basi kuna hatari ya kuilisha jamii yetu uongo. Mfano,
kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinavyotafsiriwa
kisiasa.
Bila shaka vyombo vya habari ni
kama mshipa wa damu wa siasa na demokrasia nchini. Hakuna chama cha
siasa kinachoweza kufanya siasa kwa ufanisi pasipo kushirikiana na
vyombo vya habari, hivyo waandishi wa habari wanakuwa vijumbe wa kubeba
ujumbe wa wanasiasa, kuupeleka kwa wananchi na kubeba mrejesho wa
wananchi na kuupeleka kwa wanasiasa juu ya sera na mienendo yao
Akizungumza wakati wa Semina
iliyoandaliwa kwa ajili ya waandishi wa habari kuhusu namna bora ya
uandishi wa habari za shughuli za Bunge, semina iliyoandaliwa na Ofisi
ya Habari ya Bunge kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la UNDP
ambayo ilifanyika tarehe 6 Septemba, 2014 mjini Dodoma, Mkurugenzi wa
Habari, Elimu kwa Umma na Itifaki wa Bunge Maalum, Bw. Jossey Mwakasyuka
alisema kuwa lengo la semina hiyo ilikuwa ni kuweza kujadiliana na
kubadilishana uzoefu juu ya uandishi wa habari kwa waandishi ili kuweza
kuandika habari zilizo sahihi zinazohusu Bunge hilo kwa manufaa ya
taifa.
Katika semina hiyo waandishi wengi
watakuwa wameelimika vya kutosha kwani ni mambo mengi yenye umuhimu
yaliwasilishwa na watoa mada waliobobea katika mambo ya uandishi na
siasa hali ambayo itawafanya waandishi wengi nchini kuzingatia weledi na
maadili pindi wanapokuwa wanaandika habari zinazohusiana na bunge hilo
ili kuhabarisha umma.
Katika semina hiyo, watoa mada
waliweza kugusia mambo mbalimbali yakiwemo uandishi wa habari za Bunge
na Siasa wenye tija, athari za siasa katika uandishi wa habari za Bunge,
madhara ya Vyombo vya habari kutumika, miiko na maadili ya kuzingatia
katika uandishi huo.
0 comments:
Post a Comment