Wednesday, 10 September 2014


images

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba,Askofu Mstaafu, Donald Mtetemela , ambaye yuko katika Kamati  Namba Nane ya Bunge, hilo amewashauri wajumbe wenzake kuwa suala la maadili na miiko ya viongozi na utumishi wa umma, lisiwe kwa watu hao tu bali  hata kwa jamii nzima.
 
Kauli hiyo imetolewa  leo na Askofu Mtetemela,wakati akichangia mjadala wa kujadili sura zilizobakia za Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kikao cha thelasini  na saba cha Bunge hilo linaloendelea mjini Dodoma, ambacho kinaendelea  na sura ya Pili, Tatu, Nne na Tano za Rasimu hiyo.
 
Askofu Mtetemela aliyasema hayo akiwa anachangia mjadala katika Bunge hilo, katika sura ya Tatu ya Rasimu hiyo.
 
“Ninapenda kuunga mkono taarifa ya Kamati Namba  Nne ya Bunge Maalum la Katiba ambayo ilibadilisha kichwa cha habari katika sura hii kuwa Maadili na Miiko ya Taifa. Neno maadili  lina upana. Suala la maadili si kwa watawala tu, maadili yanaanza  na jamii,” alisema Askofu Mtetemela.
 
 Aliongeza kwamba kiongozi anatoka katika jamii, hivyo ni vema jamii lazima iwe maadili.
 
“Taifa lihimize jamii kuwa na utamaduni mzuri. Taasisi kujifunzia, vyuo vya elimu na vyombo vya dini vina wajibu wa kujenga maadili katika  jamii,”alisisitiza.

0 comments:

Post a Comment