Friday 5 September 2014

 WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kufanya upya sensa ya mifugo kwani ya mwisho ilifanyika miaka 30 iliyopita.
 Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Septemba 5, 2014) wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa wadau wa mifugo hapa nchini ulioanza leo kwenye hoteli ya Malaika jijini Mwanza.
 Waziri Mkuu amesema ni vigumu kwa wafugaji kutaja idadi halisi ya mifugo waliyonayo lakini kama Wizara hawana budi kuweka mbinu za kisasa za kufanya sensa hiyo hata kama itawachukua miaka miwili.
 “Hizi takwimu kwamba Tanzania ina idadi ya ng’ombe milioni 22.8 zinaweza zisiwe sahihi sana. Sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 1984… Hizi takwimu zitakuwa ni za kutoka kwa watendaji tu hapa na pale. Na mara nyingi ukiwauliza wafugaji wanakutajia idadi ndogo wakati idadi halisi wanaificha. Tunahitaji kufanya sensa halisi ya mifugo hapa nchini,” alisema.
 Aliwaeleza washiriki wa Mkutano huo kwamba mifugo ni sekta muhimu hasa ikizingatiwa kwamba inawawezesha wananchi kupata milo yao. “Ukichukua kilimo, hakuna mtu ambaye hana kijishamba japo kidogo. Kwenye mifugo hakuna anayekosa walau kuku au bata wa kufuga, kwenye uvuvi nako watu wanaenda baharini au ziwani kila kukicha ili kupata chochote na kwenye misitu nako kuna rasilmali zinazotokana na misitu na kubwa ni zao la asali,” alisema huku akishangiliwa.
 Alisema fursa zilizopo hazitumiki ipasavyo kwa sababu watendaji wengi wamezoea kukaa ofisini badala ya kwenda waliko wananchi na kuwaelimisha jinsi wanavyoweza kunufaika na fursa hizo. “Fursa zipo nyingi, kikubwa ni kujipanga vizuri na kumwezesha Mtanzania wa kawaida atumie fursa hizo ili kubadilisha maisha yake,” alisema.
 “Tunatakiwa kumbadilisha fikra mfugaji mdogo ili aone ng’ombe alionao ni fursa. Tubadili fikra za mfugaji huyu mdogo ili aone umuhimu wa kufuga ng’ombe wachache watakaolishwa vizuri na kumpatia kipato kikubwa. Aone kuna tija katika idadi ndogo ya mifugo badala ya kufurahia uwingi wao,” aliongeza.
 Alisisitiza haja ya wataalamu kuwafundisha wafugaji aina nyingine za ufugaji badala ya kung’ang’ania ngombe tu na mbuzi. “Hivi sasa kondoo wana soko kubwa sana Uarabuni kwa sababu wanasema nyama yake haina cholesterol (lehemu). 
 “Kuna kuku wa chotara sasa hivi wanauzwa kuanzia sh.35,000/-. Mtu akiwa na kuku 100 hii ni fursa nzuri tu. Nilitembelea banda la Ukerewe kwenye maonyesho ya NaneNane hapa Mwanza, nikakuta mtu anafuga bata mzinga, kuuliza bei gani akajibu mmoja anauzwa sh. 180,000/-. Kama ni Dar es Salaam huyo bata mzinga angeuzwa kwa sh.4000,000/-. Tutumie fursa hizi, tuwaelimishe wananchi wetu ili waweze kutoka hapo walipo,” alisema.
 Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mkutano huo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani alisema licha ya kuwepo idadi kubwa ya mifugo nchini, Watanzania bado hawajaweza kufikia kiwango kinachotakiwa cha ulaji wa bidhaa za mifugo kama mayai, nyama na maziwa.
 “Mtanzania kwa wastani anakula mayai 72 kwa mwaka, lita za maziwa 45 na kilo 11 za nyama kwa mwaka wakati kiwango kinachotakiwa ni mayai 300, lita 200 za maziwa na kilo  50 za nyama kwa mwaka. Bado tuna kazi kubwa ya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kula bidhaa zinazotokana na mifugo,” alisema

0 comments:

Post a Comment