Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe leo amezindua magari 54 ya abiria
ya Chama cha Ushirika cha Madereva wa Taksi katika Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Jijini Dar es Salaam yenye thamani
ya sh. Milioni 840 kuboresha usafiri wa abiria.
Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika
katika eneo la kiwanja cha zamani cha Ndege, Terminal I, makao makuu ya
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ambapo ameiagiza TAA
kuhakikisha inaipa hadhi JNIA kama alivyokuwa mwenye jina hilo, Hayati
Mwalimu Julius Nyerere.
“TAA hakikisheni JNIA inabeba jina
la Julius Nyerere kwa mandhari, utendaji na vyombo vya usafiri, “
Waziri Mwakyembe amemweleza Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Moses Malaki na
uongozi wa TAA kwa jumla.
Waziri Mwakyembe amesema, hatua ya
ATACOS kununua magari hayo inaongeza ubora wa huduma na hadhi ya
kiwanja cha ndege cha JNIA na kwamba magari hayo yatasaidia kuchukua
hata wageni wa Serikali
Alisema mradi huo wa magari ni
mkubwa kwa wana ushirika hao na magari yao ni ya viwango vya juu na hata
kwa mbali ukiyaangalia magari hayo, yana viwango vikubwa na Serikali
ikipata wageni zaidi ya 500 kwa mpigo, haitahangika kutafuta magari
kwani hayo yapo. Thamani ya gari moja ni sh. Milioni 15 na ni mkopo wa
Equity Bank.
Hata hivyo, Waziri Mwakyembe
amewataka madereva hao kuzingatia usafi wa magari na wao wenyewe kwani
wageni wakikodi magari hayo na kuyakuta ni nadhifu na wao ni wasafi,
ndio kielelezo cha nchi yetu.
“Naheshimu sana kazi mnayofanya.
Ina add value (ongeza thamani), “ waziri Mwakyembe amesema na kuutaka
uongozi wa TAA utambue mchango wa madereva hao kwani magari yao ni
mazuri na hata katika jengo la tatu la abiria (TB III) linalojengwa,
yanaweza kupewa fursa.
Amewataka kuyatunza kwa kuyavika
vita vyeupe na wao kuvaa sare nyeupe na kusimamia viwango kwa kuwa na
zaidi ya sare moja nyeupe ili hata akiingia mtalii, ajue kuwa anaingia
nchi ya wastarabu.
Hata hivyo, Waziri Mwakyembe
ameeleza kusikitishwa na madereva hao kuushitaki uongozi wa TAA
mahakamani kuhusu haki ya kuendesha biashara ya taksi JNIA. Amewaeleza
asingeweza kuwasaidia kutatua kero hiyo kwa kuwa kuna kesi hiyo bado iko
mahakamani hadi leo.
“Sijui nani aliwashauri. Mimi ni
Kiongozi wa Serikali tena ni Wakili wa Mahakama Kuu. Siwezi kuingilia
utendaji wa mhimili mwingine wa chombo cha haki. Nitaonekana wa ajabu.
Mikono yangu imefungwa katika hili, “ aliwaeleza na kuacha kujibu kero
zao kuhusu mgogoro huo.
Katika risala yao kwa Waziri
Mwakyembe, Katibu wa stendi ya madereva teksi JNIA, Mohammed Mashombo
amemweleza Waziri mafanikio na kero zao tangu waanze 2000 na kuomba
awasaidie.
Hata hivyo, uongozi wa TAA
ulimweleza Waziri Mwakyembe awali kuwa, madereva hao waliushitaki
kuhusiana na mkataba wa kufanya biashara JNIA na kesi hiyo inaendelea
hadi leo na kwamba mengi ya madai waliyomtaka awasaidie, ndio
wameyewasilisha mahakamani.
Hafla hiyo imehudhuriwa na wageni
mbalimbali na watendaji wa TAA, Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege
Tanzania, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Meneja wa TRA Mkoa wa Temeke,
Mkurugenzi wa Equity Bank, Mkurugenzi wa ABG na Afisa Biashara wa
Manispaa Temeke.
0 comments:
Post a Comment