MOTO
mkubwa umeteketeza maduka 18 katika mtaa wa Kwakivesa wilaya ya Handeni
mkoani Tanga baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta kugonga nguzo ya
umeme kupinduka na kisha kuanza kuwaka moto uliosambaa hadi kwenye
maduka hayo.
Taharuki
hiyo imetokea leo majira ya saa 5:00 asubuhi baada ya lori hilo
lililokuwa kwenye mwendo kasi kutaka kumkwepa mwendesha bodaboda na
kujikuta likiacha njia na kugonga nguzo ya umeme na kusababisha hasara
kubwa kwa wananchi huo.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kudai kuwa moto huo ulitokea saa 5.asubuhi katika mtaa huo
kufuatia roli la mafuta aina ya Fuso kugonga nguzo ya umeme na
kusababisha betri kutoa cheche zilizosababisha moto kuanza kuwaka.
Kamanda
Kashai amesema roli hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva Ali Makelele
ambaye bado hajapatikana huku utingo wake aliyemtaja kwa jina moja la
Mfundo akiwa amekimbizwa hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa matibabu
Zaidi baada ya kuungua vibaya.
"Moto
ulianza kuliteketeza roli hilo la mafuta na baadaye ukasambaa kwenye
maduka jirani ,hali ilikuwa mbaya sana, hadi sasa hatujajua hasara
iliyopatikana, tutakapokuwa na taarifa kamili tutawataarifu", amesema
kamanda Kashai.
Aidha
mashuhuda wa tukio hilo wanaeleza kuwa moto huo ulishika kasi kwa haraka
kutokana na hali ya hewa kuwa ya upepo mkali licha ya juhudi za
wananchi kuuzima lakini uliwashinda nguvu.
Aidha
jeshi la polisi limelaani mtindo unaoota mizizi hivi sasa wa wananchi
kujichukulia sheria mkononi kwani baada ya tukio la moto kutokea kikosi
cha zimamoto kutokea Korogwe kilifika katika eneo la tukio lakini badala
ya kuachwa kufanya kazi yake kikashambuliwa.
Shambulio
hilo la wananchi kwa zimamoto limesababisha hasara ikiwa ni pamoja na
kuvunjwa vioo vya gari, kupotea kwa vitendea kazi pamoja na baadhi ya
askari wa zimamoto kujeruhiwa.
CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment