Tuesday, 2 June 2015


Vumbi la kinyang’anyiro cha uteuzi wa kuwania urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), linaanza rasmi Dodoma leo kwa wanachama wake watano kuchukua fomu wakiomba uteuzi huo.
 
CCM imepanga kuanzia leo Juni 3 hadi Julai 2, mwaka huu, kuwa siku za kuchukua na kurudisha fomu za wanachama wake wanaoomba uteuzi kuwania urais.
 
Uteuzi huo ni kwa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kwa uteuzi wa Rais wa Zanzibar, fomu zitakuwa zikitolewa kisiwani Unguja.
 
Tayari wanachama wa CCM kadhaa wamekwisha kutangaza nia ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete huku wengine zaidi wakitarajiwa kufanya hivyo.
 
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) wa Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatib, uchukuaji wa fomu hizo unaanza rasmi leo.
 
Khatib aliwaambia waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya CCM ‘White House’, Mtaa wa Nyerere mjini Dodoma  kuwa fomu zitaanza kutolewa saa nne asubuhi.
 
Alisema kwa mujibu wa orodha waliyonayo, wanachama watano watachukua fomu hizo kuanzia saa nne asubuhi hadi saa 10:30 jioni, na kila mmoja amepewa saa moja na wametenga muda wa kuzungumza na waandishi wa habari kwa wagombea ambao wataona inafaa kwao.
 
“Uchukuaji huu wa fomu haukufuata umaarufu wa mtu, ujuzi, alfabeti, nafasi yake katika Chama na Serikali, bali umefuata aliyewahi kutoa taarifa kwa Chama,” alisema Khatib akifafanua uchukuaji huo.
 
Alimtaja wa kwanza kuchukua fomu kuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya kuanzia saa 4 kamili hadi saa 5:30.
 
Profesa Mwandosya atafuatiwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira kuanzia saa 5:30 na atafuata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa atachukua fomu kuanzia saa saba kamili.
 
Wa nne atakuwa Waziri wa zamani wa Muungano, Balozi Amina Salum Ali kuanzia saa 8:30 mchana na pazia la ufunguzi litafungwa saa 9:30 alasiri na mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Charles Makongoro Nyerere.
 
Mbali ya wanachama hao watano, wanaCCM wengine ambao wametangaza nia ya kuwania urais ni Lazaro Nyalandu, Frederick Sumaye, Profesa Sospeter Muhongo, January Makamba, Mwigulu Nchemba na Luhaga Mpina.
 
Wanaotajwa ni pamoja Bernard Membe, William Ngeleja, Dk Titus Kamani, Luhaga Mpina, Mizengo Pinda, Dk Asha-Rose Migiro, Shamsi Vuai Nahodha, Dk Emmanuel Nchimbi na Dk Hamis Kigwangalla.
 
Katibu huyo wa Oganaizesheni alisema uchukuaji huo wa fomu utazingatia taratibu zilizowekwa na CCM na kutakuwa na fomu tatu zitakazopewa wagombea.
 
Fomu ya kwanza itahusu maelezo binafsi ya mgombea, itahusu uzoefu na ujuzi wake, nyingine itakuwa ya kujaza orodha ya wadhamini wake na nyingine ya masharti kama yalivyokubaliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa,” alifafanua Dk Khatib.
 
Alisema katika wadhamini, mgombea atatakiwa kupata wadhamini 450 kutoka katika mikoa 15 ya Tanzania Bara na mikoa mingine mitatu ya Tanzania Zanzibar.
 
“Mjumbe yeyote wa Mkutano Mkuu wa Taifa haruhusiwi kumdhamini mgombea, pia mwanachama haruhusiwi kudhamini mgombea zaidi ya mmoja,” alifafanua.
 
Alisema ili kuonesha uhalali wa fomu hizo za wadhamini, zitapaswa kuwa na mhuri wa Katibu wa CCM wa wilaya husika pamoja na saini yake na pia mdhamini atapaswa kusaini na kuandika kadi yake ya uanachama.
 
Alisema wagombea hao watakapofika kuchukua fomu, wanapaswa kuwa na ada ya Sh milioni moja na watasaini daftari maalumu kuonesha ndio waliochukua fomu.
 
“Tumepanga muda wa saa moja moja na nusu kwa kila mgombea kuwapo hapa. Na akishachukua fomu tumepanga anayetaka azungumze na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa NEC,” alisema Dk Khatib.
 
Alisema katika chumba cha uchukuaji wa fomu, wataruhusiwa mgombea kuingia na watu wasiozidi 10.
 
 “Katika chumba hiki (cha mikutano na waandishi katika Makao Makuu) tutaruhusu mgombea kuingia na watu wasiozidi 10… mkewe na jamaa zake wengine, wanaomsindikiza, sijui wengine mnawaita wapambe, mimi nawaita wanaomsindikiza,” alisema Katibu huyo.
 
Aliwataka wagombea wengine wanaotaka kuchukua fomu hizo kuwasiliana mapema na ofisi yao kwani alisema wangependa kazi ya uchukuaji fomu kudumu kwa siku zisizozidi tano ili shughuli nyingine ziendelee.
 
“Tunawaomba wagombea wengine wanaotaka kuja kuchukua fomu kufanya hivyo mapema. Tungependa ndani ya siku tano tuwe tumemaliza ili shughuli nyingine ziendelee kwani hata wao wana kazi ya kutafuta wadhamini mikoani,” alifafanua kiongozi huyo mkongwe

0 comments:

Post a Comment