Saturday, 30 May 2015

Ndugu Gratian Mukoba, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, TUCTA;Mhe. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Mheshimiwa Gaudencia Kabaka, Waziri wa Kazi na Ajira;
Mheshimiwa Celina Kombani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma;
Mheshimiwa Hamis Majaliwa, Naibu Waziri – TAMISEMI;
Mheshimiwa Margaret Sitta, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Jamii;
Mhe. Felix Daud Ntibenda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Ndugu Msulwa, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania;
Ndugu Nicholaus Mgaya, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, (TUCTA);
Ndugu Ezekiel Oluoch, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania;(P.T)
Ndugu Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha Walimu Tanzania;
Mke wangu Mama Salma Kikwete;
Ndugu Walimu;
Wageni waalikwa;
Shukurani
Nakushukuru sana Rais wa Chama cha Waalimu Tanzania (CWT) Ndugu Gratian Mukoba na viongozi wenzako wa CWT kwa kunialika na kunipa heshima kubwa ya kufungua Mkutano wenu Mkuu. Nawapongeza kwa maandalizi mazuri ya mkutano. Kufanikisha mkutano wa Wajumbe 1,200 si kazi ndogo hata kidogo. Hivyo basi unapofanikiwa ni jambo linalostahili pongezi. Hongereni sana. Pia nikushukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Arusha na wananchi wote wa Mkoa huu kwa mapokezi mazuri na kwa kukubali kuwa wenyeji wa mkutano huu. Mmekuwa wenyeji wema. Hongereni sana.
Pongezi kwa CWT
Ndugu Rais
Ndugu Waalimu;
Natoa pongezi kwa viongozi wa Chama cha Waalimu wanaomaliza muda wao kwa kazi kubwa nzuri waliyofanya na kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana na yanayoendelea kupatikana. Mmeifanya vyema kazi ya kutetea haki na maslahi ya walimu. Tumejionea jengo kubwa na zuri la kitega uchumi lililojengwa Ilala, Dar es Salaam. Jengo hili lijulikanalo kama Mwalimu House limependezesha sana eneo la Ilala na jiji la Dar es Salaam. Kama kwamba hiyo haitoshi hivi karibuni tumepokea habari nyingine njema za kuanzishwa kwa Benki ya Waalimu itakayojulikana kama Mwalimu Bank. Mafanikio haya na mengine mengi ambayo sikuyataja, yanafanya CWT kuwa moja ya vyama vya wafanyakazi mahiri na makini nchini licha ya kuwa ndicho Chama kikubwa kuliko chote chote. Hongereni sana viongozi na wanachama wa CWT.
Risala ya Chama cha Waalimu
Ndugu Rais
Ndugu Waalimu;
Nimeisikia na kuipokea risala yenu nzuri mliyoiwasilisha kwangu muda mfupi uliopita. Nawashukuru kwa risala yenu imeainisha mafanikio, mliyopata, changamoto zinazowakabili na muhimu zaidi mmetoa ushauri muafaka kuhusu namna bora ya kuzitatua. Ni risala inayotoa fursa ya kujadiliana na kushirikiana na yenye lengo la kujenga na kuimarisha mahusiano ya pande zetu mbili. Ni risala inayoonyesha kuwepo kwa kushirikiana, kustahamiliana na kuaminiana kati ya walimu na Serikali yao. Sisi sote inatupa funzo kuwa, pale panapokuwepo na uhusiano mzuri na ushirikiano kati ya walimu na Serikali, haliharibiki jambo. Hata yale mambo ambayo pengine yalionekana magumu, tumeweza kuyatatua kwa pamoja. Hatuna budi kuendeleza hali hii ya mahusiano kati yetu siku zote.
Risala yenu pamoja na mambo mengine imeibua masuala tisa. Masuala hayo ni kuhusu madaraja ya walimu; posho ya kufundishia; madeni ya walimu; uhaba wa nyumba za walimu; utoaji wa elimu bora; mabadiliko ya mafao ya pensheni; ukaguzi wa shule; Sekta ya Elimu katika BRN; na mapungufu ya kiutendaji katika kuhudumia walimu. Mambo yote haya ni ya msingi sana na yanastahili kupatiwa majawabu muafaka. Yapo ya kisheria, ya kisera na ya kimfumo. Napenda kuwahakikishia kuwa nimeyapokea na tutayafanyia kazi mambo yote kama kawaida yetu. Kama mlivyosema katika risala yenu, baadhi ya mambo yanahitaji kukaa mezani kujadiliana na kushauriana zaidi. Tutafanya hivyo. Nitajitahidi kwa yale yanayowezekana niwe nimeyatatua kabla ya kumaliza muda wangu wa uongozi. Kwa yale ambayo yanahitaji muda mrefu, nitahakikisha kuwa kabla ya kukabidhi ofisi niwe nimeyawekea msingi mzuri ili iwe rahisi kwa Rais ajaye baada yangu kuyakamilisha.
Hatua za Serikali Kushughulikia Madai ya Waalimu
Ndugu Rais na
Ndugu Waalimu;
Kwa uchache, nitapenda kuzungumzia hatua ambazo Serikali imechukua na inazoendelea kuchukua kushughulikia madai ya waalimu. Kama mlivyoainisha katika risala yenu, Serikali ninayoingoza imefanya jitihada kubwa sana kupanua fursa za watoto wetu kupata elimu na sasa tumeelekeza nguvu zetu katika kuboresha elimu inayotolewa. Kwa ajili hiyo, tumeongeza shule za msingi kutoka 14, 257 mwaka 2005 hadi 16, 343 mwaka 2014, na kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka milioni 7.54 hadi milioni 8.23. Shule za Sekondari, zimeongezeka kutoka 1,745mwaka 2005 hadi 4,576 mwaka 2014 na kuongeza wanafunzi kutoka 524, 325 hadi milioni 1.8 kati ya mwaka 2005 na 2015. Hali kadhalika, idadi ya vyuo vikuu imeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi 52 mwaka 2015, na kufanya idadi ya wanafunzi kuongezeka kutoka 40, 719 hadi200, 986 katika kipindi hiko.
Sote tunafahamu kuwa shule na elimu haikamiliki pasipo na waalimu na pasipokuwa vitabu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Upanuzi huo mkubwa ulilazimu kupanua vyuo vya ualimu. Idadi ya vyuo vya ualimu vya cheti na stashahada vimeongezeka kutoka 52 mwaka 2005 hadi 126mwaka 2015. Upanuzi huu ukiongeza na ule wa vyuo vikuu umewezesha kuongeza idadi ya waalimu wa msingi na sekondari kutoka 153, 767mwaka 2005 hadi 301,960 mwaka 2015. Hii imewezekana kutokana pia na uamuzi wetu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi waliochagua kusomea ualimu, na kuwahakikishia ajira pale wanapomaliza masomo yao.
Serikali imefanya jitihada pia za kuboresha maslahi ya waalimu kadri uwezo uliporuhusu. Hatukuweza kutoa nyongeza kubwa kwa wakati mmoja lakini tumeongeza mara kwa mara. Kati ya 2005 – 2015 kumekuwepo na ongezeko la kianzio cha mshahara cha Mwalimu mwenye cheti, Mwalimu mwenye Stashahada ya Ualimu na wale wenye elimu ya shahada. Watumishi wa kada nyingine za Serikali wenye elimu ya viwango hivyo, huanza na mshahara wa chini ya ule wa waalimu. Nafahamu kuwa kiwango hiki bado hakitoshi, lakini ukweli ni kuwa hakuna upungufu wa dhamira kwa upande wa serikali, ila kikwazo ni kutokuwepo na uwezo mkubwa kimapato kwa upande wa Serikali. Ukizingatia kuwa walimu ni asilimia 52.7 ya watumishi wa Serikali, hivyo, ongezeko katika mshahara wa waalimu linaleta mabadiliko makubwa sana katika bajeti ya Serikali. Kwa ajili hiyo hatukuweza kutoa nyongeza kubwa kwa wakati mmoja lakini tumeongeza mara kwa mara mpaka tumefikia hapa tulipo leo. Na katika bajeti hii tutaongeza tena. Hivyo nitawaacha mahali penye unafuu ukilinganisha na tulikotoka.
Tumeendelea pia kushughulikia kero nyingine za waalimu ikiwemo madeni na madai yenu. Deni la waalimu lililopokelewa lilikuwa shilingi bilioni 53, 185,440,406 lililohusu waalimu 70,668. Baada ya uhakiki uliofanyika kwa kuhusisha Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali, jumla ya shilingi bilioni 23, 233, 654, 025 zililipwa kwa waalimu 29,243. Serikali imeshatoa ahadi ya kulipa ifikapo mwezi Agosti mwaka huu madai mengine ya waalimu 7,169 yenye jumla ya shilingi bilioni 9, 285,283,600 ambayo uhakiki wake umekamilika. Aidha, madai ya walimu 30,807yenye jumla ya shilingi bilioni 17,346, 593, 468 hayakuweza kulipwa kutokana na kukutwa na dosari za msingi za kihasibu na kiutaratibu. Wametakiwa kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Jambo la kururahisha katika ukaguzi na uhakiki huo wa madeni ni kule kushirikishwa kwa Chama cha Walimu. Kwa pamoja tumethibitisha palipokuwa sahihi na pasipokuwa sahihi. Inasikitisha kupata taarifa za kuwepo vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Serikali na walimu vinavyochangia kuzalisha madeni bandia. Vitendo vyao hivyo ndivyo vinavyofanya madai yachukue muda mrefu kulipwa kwa kulazimika kuweko na uhakiki wa ziada. Naungana nanyi katika pendekezo lenu la kutaka watumishi hawa kuwajibishwa, maana ndio mzizi wa fitna kati ya waalimu na Serikali. Nimekwishaeleza mamlaka husika kufanya hivyo bila ajizi.
Ndugu Rais na
Ndugu Waalimu;
Tumeshughulikia lile dai kubwa la waalimu la marekebisho ya muundo wa utumishi wa waalimu (Teacher's Service Scheme). Tumepitisha Muundo mpya wa Waalimu ambao umeanza kutumika toka Julai 1, 2014. Nimesikia kuwa utekelezaji wake haukuweza kuanza kote nchini mara moja, napenda kuwahakikishia kuwa katika mwaka ujao wa fedha tutahakikisha kuwa Waalimu wote watakuwa wamefikiwa. Sambamba na hili la Muundo, tumekwishapeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya kuanzisha Tume ya Utumishi wa Waalimu (Teachers Service Commission) ambao tayari umesomwa kwa mara ya kwanza. Mawasiliano yanaendelea na Ofisi ya Spika ili Muswada huo ujadiliwe katika Bunge hili la Bajeti. Tunafanya hivyo pia kwa Muswada wa kuanzisha Bodi ya Taifa ya Taaluma ya Waalimu (Teachers Proffessional Board). Nimepokea maoni yenu ya kutaka uangaliwe uwezekano wa Bodi hii kuwa sehemu ya Tume ya Utumishi wa Waalimu badala ya kuwa na vyombo viwili tofauti. Hoja yenu ya kutaka kupunguza utitiri wa vyombo vinavyoshughulikia maslahi ya waalimu ina mashiko. Ushauri wenu umepokelewa, tutautafakari na kuufanyia kazi.
Napenda kuwahakikishia kuwa madai yenu mengine ikiwemo nyumba za waalimu, motisha kwa waalimu, mazingira ya kufanyia kazi, mafunzo vikokotoo vipya vya pensheni na masuala mengine mliyoibua katika risala yenu tutayashughulikia na tutawapeni taarifa. Pia nitaelekeza mamlaka zinazohusika kukutana na uongozi mpya wa Chama chenu baada ya uchaguzi mkuu wenu kuyajadili masuala hayo na kuyatafutia majawabu.
Napenda kusisitiza kwenu kwamba mimi na wenzangu Serikalini tunawathamini sana na kuwapenda waalimu kwa dhati ya mioyo yetu. Sisi tunatambua nafasi ya Mwalimu katika maendelo ya mtu binafsi na taifa kwa jumla. Hakuna badala yake. Hivyo basi tunatambua wajibu wetu wa kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Tumefanya jitihada kutimiza wajibu wetu. Pale panapojitokeza matatizo yoyote si makusudio yetu. Kitendo cha makusudi na anapojulikana mtu huyo atawajibishwa ipasavyo. Wakati mwingine matatizo yanayowakuta hutokana na watu wetu kuelemewa na mzigo kutokana na ukubwa wa kada yenu katika utumishi wa umma ambapo ni asilimia 52. 7.
Kwa ukubwa huu, mnaweza kuelewa ni changamoto kiasi gani zinazojitokeza katika kushughulikia masuala yenu. Ndio sababu hatuchoki kutafuta muundo bora wa kushughulikia matatizo yenu. Ninachoomba kutoka kwenu ni uvumilivu na uelewa wenu na kuwaomba mtupime kwa dhamira yetu na utayari wetu wa kuyashughulikia madai yenu na si kwa idadi ya changamoto zinazojitokeza.
Uchaguzi Mkuu wa CWT
Ndugu Rais na
Ndugu Waalimu;
Moja ya Agenda kubwa ya Mkutano wa leo ni Uchaguzi Mkuu. Nitumie fursa hii kuwapongeza viongozi mliochaguliwa katika ngazi ya Tawi, Wilaya na Mkoa ambao kwa pamoja mmeunda Mkutano Mkuu huu. Nawapongeza kwa kuuendesha uchaguzi wa ngazi za chini vizuri maana natambua kuwa haikuwa kazi ndogo kutokana na ukubwa wa nchi yetu, na hamasa ya waalimu kisiasa.
Nawapongeza sana viongozi wote waliojitokeza kugombea nafasi za uongozi wa ngazi ya Taifa. Naamini nyote mnatosha kwa nafasi mnazoomba. Naomba mkumbuke kuwa si kila mtu aliyeomba atashinda. Nafasi si nyingi kiasi hicho. Hivyo basi, wale ambao kura hazitatosha safari hii, watumie uzoefu walioupata katika uchaguzi huu kujinoa zaidi kwa chaguzi za miaka ijayo. Haitakuwa vizuri iwapo wale ambao hawatafanikiwa kushinda, wataendeleza nongwa na kuwa chanzo cha kuvunja mshikamano mzuri mlionao katika Chama cha Walimu. Kama nilivyosema awali, sisi sote tunawaangalia waalimu kama kioo cha maadili na upevu katika jamii yetu. Naamini hamtatuangusha.
Nawapongeza na kuwashukuru sana viongozi wanaomaliza muda wao kwa ushirikiano wenu mkubwa mliotupatia sisi katika Serikali katika kipindi chenu cha uongozi. Kwa pamoja tumeweza kutatua changamoto nyingi za waalimu na kujenga madaraja kati yetu yaliyozaa mahusiano mazuri ambayo ndio msingi wa kutatua madai ya waalimu kila yalipojitokeza. Ni matumaini yetu kuwa viongozi watakaochaguliwa, wataendeleza pale mlipoishia na muhimu zaidi uhusiano mzuri na ushirikiano na Serikali. Sisi tunaahidi kuwapa kila aina ya ushirikiano unaostahili. Ni jambo lenye maslahi kwetu sote.
Hitimisho
Ndugu Rais na
Ndugu Waalimu;
Hii ni fursa yangu ya mwisho kukutana na kuzungumza na viongozi wa CWT nikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya hapo nitakuja kumsindikiza Mwalimu mwenzenu akija mkutanoni. Hivyo, sina budi kutumia fursa hii pia kuagana nanyi na kupitia kwenu kuagana na Waalimu wote nchini. Nirudie tena kuwashukuru sana kwa mchango wenu mkubwa katika maendeleo ya elimu nchini. Kwa kweli mnajitoa sana na mnafanya kazi kubwa ambayo inaonekana na wote. Napenda kuwatia moyo kuwa msilegeze uzi bali muendelee na moyo na wito wenu huo. Nitawakumbuka sana waalimu katika maisha yangu baada ya kustaafu uongozi, kwa msaada wenu na ushirikiano wenu. Nimewapenda, ninawapenda na nitaendelea kuwapenda 'Shemeji' zangu.
Nawatakia Uchaguzi Mkuu na Mkutano Mkuu mwema.
Akhsanteni kwa kunisikiliza!

0 comments:

Post a Comment